Saturday, October 4, 2014

Samuel Sitta, Nisingeshiriki Kalamu Ya Wenye Dhambi.

Mheshimiwa Samuel Sitta.
Kwako mheshimiwa Samuel Sitta.
Ni matumaini yangu kwamba sasa unajipongeza kwa kufanikisha kazi uliyopewa ya kuliongoza Bunge Maalum la Katiba ya kuhakikisha akidi inatimia ili kupitisha rasimu ya katiba inayopendekezwa.

Najua una furaha sana kwa hilo, upo kwenye karamu ya kufurahia ushindi kiasi kwamba itakuwa vigumu sana kwa lofa kama mimi kukutana na wewe hasa katika kipindi hiki ambacho unaamini kasi na viwango vyako vimedhihirika. Hata hivyo, hilo halinizuii kufikisha ujumbe wangu kwako.
Mimi si Mbunge wa Urambo Mashariki kama wewe, sikuzaliwa Desemba 18, 1942 wala sijamuoa mwanamke mwanasiasa, Magreth Sitta aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikali kama wewe. Mimi ni mwananchi wa kawaida tu, lofa, hohehahe nisiye na mbele wala nyuma.
Sijawahi kuwa spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wala sijawahi kujipatia umaarufu mkubwa na kupendwa na wengi kutokana na kuruhusu mijadala ya ufisadi bungeni kama ulivyo wewe. Sijawahi kuibua kashfa kubwa kama ya Richmond na kusababisha baadhi ya vigogo wang’atuke kwenye nyadhifa zao.
Sina nia wala sitegemei kuja kugombea urais wa nchi hii kama wewe, mimi ni mwananchi wa kawaida kabisa. Sijawahi kujisifu kwamba mimi ni mtu wa viwango na kasi, mimi ni mlala hoi tu.
Sijawahi kuitumia nchi hii katika nyadhifa mbalimbali kuanzia nilipokuwa shule, kwa zaidi ya miaka 40 nikigusa karibu awamu zote za uongozi kama wewe, mimi si Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wala sijawahi kuota ndoto kwamba nitakuja kuwa Spika wa Bunge Maalum la Katiba! Narudia tena, mimi ni mwananchi wa kawaida kabisa, hohehahe nisiye na ndoto za kuja kuwa mwanasiasa.
Hata hivyo, ningekuwa mimi ndiyo nipo kwenye nafasi yako, hakika nakuapia nisingeshiriki kwenye karamu ya wenye dhambi kama wewe. Nisingeshiriki hata kidogo kuchakachua maoni ya mwenyekiti wa tume ya kukusanya maoni kuhusu katiba mpya, Jaji Joseph Warioba kama wewe.
Nisingerudia kukusanya upya maoni kwa wananchi wakati nikijua fika kuwa hiyo siyo kazi yangu. Nisingebadilika ghafla kama wewe, kutoka kuwa shujaa wa kutegemewa kama ulivyokuwa kipindi ulipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na kuwa adui wa demokrasia kama ulivyo sasa.
Nakuhakikishia nisingeshiriki kabisa karamu ya wenye dhambi, kwa kulazimisha wajumbe wa bunge maalum la katiba, hata kwa vitisho waipigie kura ya ndiyo rasimu ya katiba inayopendekezwa huku nikijua waziwazi kwamba nimeshiriki kunyofoa vipengele vyote muhimu ambavyo wananchi walivipendekeza ili kupata katiba bora.
Nisingefikia hatua ya kuwatusi viongozi wa dini ambao walikuwa wakinionesha waziwazi kwamba nilichokuwa nakifanya kwenye bunge maalum la katiba hayakuwa matakwa ya Mungu bali ya watu wachache wenye dhambi.
Kwa kuwa najua kwamba katiba ndiyo ‘injini’ ya maendeleo ya taifa lolote, ningekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba maoni ya wananchi ndiyo yanayoingia kwenye katiba bila kuchakachuliwa. Ningethibitisha kwa vitendo kwamba mimi ni mtu wa kasi na viwango!
Nisingekubali kuongozwa na tamaa ya kuja kuwa rais wa nchi hii kiasi cha kulipua mchakato mzima wa kupata katiba kwa maslahi yangu na chama changu kwa sababu ningejua kwamba umri umeshanitupa mkono (Una miaka 71 sasa) lakini wapo wanangu, wajukuu na ndugu zangu wengi na watu wanaoniamini ambao wanaisubiri kwa hamu katiba mpya itakayowakomboa, baada ya ile ya awali kushindwa kuwatatulia kero zao kwa zaidi ya miaka hamsini sasa.
Narudia tena, nisingeongozwa na tamaa ya madaraka, upendeleo kwa chama changu wala maslhai ya mtu au watu fulani, la hasha! Ningesimamia haki katika ukamilifu wake na rasimu ambayo ingepatikana, ingekuwa ni mawazo ya wananchi wote na siyo uhuni kama uliofanyika sasa kupata rasimu ya katiba inayopendekezwa.
Ningeongozwa na hofu ya Mungu na nisingewaangusha wananchi ambao kwa kipindi kirefu waliniona mpiganaji ninayesimamia maslahi yao na taifa kwa jumla na kamwe nisingeshiriki karamu ya wenye dhambi kama ilivyotokea kwenye Bunge Maalum la Katiba. 
Kwa bahati mbaya mimi nitabaki kuwa mimi na sitaweza kuwa wewe lakini kama ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, kwa jinsi hali ilivyo sasa, narudia tena kusema bila kumung’unya maneno kwamba nisingeshiriki kwenye karamu ya wenye dhambi kama wewe, ningesimamia ukweli, haki na demokrasia bila kumpendelea wala kumkandamiza mtu yeyote.
Wasalaam!CHANZO GLOBAL PUBLISHER TANZANIA

No comments:

Post a Comment