Miss Tanzania 1999, Hoyce Temu amewapiga bao ma-miss wengine wote waliowahi kushikilia taji hilo baada ya kunaswa mitaani a.k.a uswazi kwa mara nyingine akijitolea katika kazi za kijamii na kuwasaidia watu wenye matatizo kupitia kipindi chake cha Mimi na Tanzania kinachorushwa kupitia Runinga ya Channel Ten. Tukio hilo liliajiri wiki iliyopita, mwanadada huyo alipoitembelea kwa mara nyingine familia ya watoto walemavu ya Mzee Samgweno iliyopo katika Kijiji cha Makuyu huko Mvomero, Morogoro ambapo kuna watoto watano waliozaliwa walemavu wakiwa hawajiwezi kwa chochote.
Hoyce siku hiyo alifika katika mtaa wanaoishi watoto hao kisha alizama jikoni, akatumia jiko la kuni kupika chakula cha familia hiyo.
Chakula kilipokuwa tayari, Hoyce, bila kujali kuchafuka, alikaa chini na familia hiyo akagonga nao mnuso huku wakicheza michezo mbalimbali.
Pamoja na kufanya yote hayo, Hoyce akishirikiana na Kampuni ya Global Publishers, walikusanya kiasi cha Sh. milioni moja na zaidi kwa ajili ya familia hiyo ambayo kwa siku wanashindia mlo mmoja tu.
“Nimefarijika sana kupika na kula pamoja na familia hii, naona ni kitu muhimu katika maisha yangu. Wakati mwingine nilikuwa sitaki kuondoka, nilitaka kuendelea kukaa nao ili kuwafariji,” alisema Hoyce.
Hii ni mara ya pili kwa Hoyce kuwatembelea, kuwapikia na kula pamoja na watoto hao walemavu.
Hoyce ni mrembo anayeshikilia rekodi ya kuwa karibu zaidi na jamii ya watu wenye matatizo mbalimbali tangu atwae taji la miss Tanzania takribani miaka 12 sasa lakini ni kama ndiyo kwanza katwaa taji hilo mwaka jana kwa jinsi anavyojitoa kwa jamii. Mungu amzidishie aishi miaka tele.(source:globalpublishers)
No comments:
Post a Comment