Wednesday, September 10, 2014

Harusi Ya Lucy Komba Yaandamwa Na Mikosi, Watumbukia Baharini Na Boti, Waokolewa.


Ndoa iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu ya nyota wa filamu Tanzania, Lucy Komba na mzungu wake raia wa Denmark anayejulikana kwa jina moja la Janus hatimaye imefungwa na kutawaliwa na matukio yenye mikosi kibao.

, Lucy Francis Komba na mzungu wake raia wa Denmark anayejulikana kwa jina moja la Janus wakiwa ni wenye furaha wakati wa harusi yao.
Ndoa hiyo ilifungwa Jumamosi iliyopita kwenye Kanisa la Roman Katoliki Parokia ya Mtakatifu Benedict lililopo maeneo ya Kurasini- Bandari jijini Dar.
Baada ya zoezi hilo kumalizika, wawili hao na wapambe wao walikwenda katika Kisiwa cha Bongoyo, Dar kwa ajili kupiga picha za ukumbusho. Kisiwa hicho kipo Kilomita 2.5 kutoka Pwani ya Jiji la Dar.
Hata hivyo, zoezi la kwenda kupiga picha kwenye kisiwa hicho liliingia mkosi kufuatia maharusi hao kupanda  boti maeneo ya Slip Way, Oysterbay, Dar na kupigwa na mawimbi makubwa yaliyowafanya watumbukie baharini kabla ya kuokolewa na wapiga mbizi mahiri.
“Jamani sijui balaa gani hili? Yaani tumetumbukia baharini tukienda Bongoyo, viatu vimezama, nguo tulizovaa zimelowa,  tukaletewa nyingine, simu yangu pia iliingia majini lakini tunamshukuru Mungu tuliokolewa na kuendelea na safari,”alisema Lucy akizungumza na Globalpublishers
Lucy alisema walifika salama kisiwani Bongoyo na kupiga picha mbalimbali za ukumbusho na baada ya kumaliza walianza safari ya kurejea mjini ili kwenda kula na watoto yatima wa Kituo cha New Life kilichopo Kigogo jijini Dar lakini wakapata mkosi wa pili.
Lucy alisema hajui ni nini, kwani alishangaa sana baada ya kutoka Bongoyo wakiwa maeneo ya Kinondoni kuna gari lililoonekana kuwafuatilia toka mbali, liliwafikia na kuligonga gari lililokuwa katika msafara wake waliokuwa wakichukua matukio kwa kamera ya video, wakashuka na kuanza kuwafanyia fujo kisha wakawapora kamera hiyo na kuondoka kwa kasi eneo hilo.
Wanaharusi Lucy Komba na mumewe Janus wakipozi kupata picha ya ukumbusho.
“Sijajua mpaka sasa wale watu ni akina nani na walikuwa na dhamira gani, sijui walitumwa? Nashindwa kuelewa maana walikuwa mabaunsa wawili na mwanamke mmoja,” alisema Lucy.
Mbali na misukosuko yote waliyopata siku hiyo, lakini maharusi hao walifanikiwa kufika katika Ukumbi wa Makumbusho uliopo Posta Mpya, Dar ambapo sherehe ya kifahari ilifanyika na kuhudhuriwa na marafiki wa bi harusi na viongozi kutoka serikalini.
Mbali na yote, shughuli hiyo ilikuwa na vituko mbalimbali ambavyo viliwakosha waalikwa, ikiwemo watu wa kareti kutoa salamu zao za kikomandoo, mtu wa mazingaombwe ya nyoka, wanenguaji kutoka Kampuni ya Bia ya Windhoek kutoa shoo ya nguvu na msanii mkongwe Bongo, Ummy Wenceslaus ‘Dokii’ kutumbuiza.
Maharusi wakiingia katika Ukumbi wa Makumbusho ulio Posta kwa ajili ya sherehe.
Bwana harusi naye alionesha mila ya kikwao kwa kulazwa chini na kuvuliwa viatu kisha kuvalishwa tena ikiwa ni ishara kwamba ameagana na ukapera.
Msanii huyo alipata zawadi kedekede kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki zake. Mama yake mzazi aliyekuwa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi, Ilala, Marietta Minangi  alimzawadia kiwanja kilichopo Bunju jijini Dar huku baba yake mdogo (jina halikupatikana) akimpa mbuzi na ng’ombe wawili wa maziwa.Kaka yake alimkabidhi shilingi milioni tisa taslimu ukumbini hapo na kamati ya sherehe ilimpa shilingi milioni tatu bila kumsahau Dokii ambaye alimzawadia matofali 500 na mifuko 10 ya simenti.
Kutokana na thamani kubwa aliyonayo mzazi wake kwa kumzaa na kumlea vyema, Lucy alimfanyia ‘sapraizi’ mama yake huyo kwa kumpa zawadi ya gari aina ya Toyota Prado ambalo alimkabidhi mahali hapo.
“Namshukuru sana mama yangu kwa malezi mazuri aliyonipa mpaka sasa nimeolewa, sioni cha kumlipa kwa thamani kubwa aliyonayo kwangu, ila nimeamua kumzawadia gari aina ya Prado, japo ana gari lakini nimemzawadia hili ikiwa kama upendo wangu kwake,”alisema Lucy ambaye siku si nyingi anataraji kuondoka nchini kwenda Denmark kwa mumewe.

Source: Globalpublishers


Like our Facebook page Swahili World Planet for more updates about Tanzanian movie stars' latest gossips, news, fashions, music plus Hollywood, Bollywood and Nollywood news.


No comments:

Post a Comment