Saturday, July 19, 2014

Makala Fupi Toka Kwa Ignas Mkindi Kuhusu Tasnia Ya Filamu Nchini Tanzania.

Hii imeandikwa na Ignas Mkindi ambaye ni mmoja wa wanaharakati na wanamapinduzi katika tasnia ya filamu Tanzania, mara nyingi nimekuwa nikivutiwa na kile anachokiandika kwenye facebook and wakati mwingine naweza kutoa comment yangu au kama sina nakaa kimya tu. Ignas ni mtu mwenye upeo pia kuhusu tasnia ya filamu nchini na huifuatilia kwa ukaribu..........


"UMOJA KATIKA TASNIA, nijuavyo mimi!!!
Mchakato wa uanzishwaji wa umoja wa wadau wa filamu kwangu ulianzia wakati wa mkutano wa marekebisho ya sheria namba 4 ya filamu ya 1976 uliofanyika uwanja wa uhuru (zamani taifa) mwaka 2009. Serikali kupitia bodi ya filamu ilitoa ushauri kuwa iundwe kamati maalumu yenye wawakilishi kutoka kila kundi la wadau.

Lengo la kamati hiyo ilikuwa ni kuangalia kiundwe chombo cha aina gani kutokana na mazingira ya Tanzania na kujifunza kutoka katika mashirikisho ya nchi zilizoendelea katika tasnia ya filamu. Katika uundwaji huo, waigizaji walitaka kufanya ujanja wa kuihodhi kamati hiyo na baada ya kugundua hilo, viongozi wa wizara wakaagiza makundi yote yakae kwa wakati mmoja na kila kundi lichague mwakilishi. Kamati ikaundwa chini ya uenyekiti wa mwanasheria wa serikali katika wizara ya habari, utamaduni na michezo.

Baada ya kushindwa kuihodhi kamati, waigizaji walienda kukaa kivyao na kuanzisha harakati zao kwa kukitumia kipindi kimoja cha runinga na kwa ufadhili wa kampuni mojawapo iliyokuwa na nguvu katika usambazaji. Hoja yao ilikuwa eti ‘’serikali ina mpango wa kupiga marufuku wasio na elimu filamu’’. Kutokana na propaganda hizo wakapata wafuasi wengi kutokana na ukweli kuwa wadau wengi wa filamu hatuna elimu, ikawa kama wanapigania haki yao.

Wengi waliwaunga mkono bila kujua kama msambazaji aliokuwa anaweka nguvu zake alikuwa kweli ana nia ya kuwasaidia wajikomboe ama lah? Tukaona shutuma nyingi sana kuelekezwa COSOTA na Bodi ya filamu kwa hoja zenye misingi ya kutetea msambazaji na siyo msanii, na sisi tuliokuwa hatuafiki tulionekana ni wale wale wanaojifanya wasomi kutaka kudhulumu tasnia ya filamu.
Wakati hayo yakiendelea kwa wadau, serikalini likaibuka jingine, watu wa BASATA wakanusa fursa zilizopo katika filamu wakasema uanzishwaji wa mashirikisho ni jukumu lao. Ukatokea mvutano mkubwa hatimaye maridhiano yakafikiwa kuwa BASATA waendelee na mchakato na kamati iliyoundwa na bodi ikavunjwa rasmi.

Naamini mambo mengi yanayoonekana sasa yangeonekana wakati kamati inaangalia ni mfumo gani unafaa na kuna changamoto zipi ila haikupewa nafasi kutokana na watu kutoelewa, sitaki kuamini kama ni tamaa za madaraka au siasa.
Kilichotokea kikatokea ikaundwa TAFF. Baada ya wanaharakati wale kukosa tena nafasi ya kuihodhi TAFF wakarudi msituni na kuendelea na yao. Sijui kilitokea nini lakini mwelekeo wa tasnia ukaonekana kama ni vita kati ya waliokuwa wakionekana kama mastaa na wale waliokuwa wanaitwa chipukizi. Nadhani kuna mtu aliwaaminisha wafuasi wake kuwa ili wafanikiwe ni lazima wagombane na upande wa pili.

Wakati fulani msambazaji aliokuwa anasapoti harakati za walioonekana kama wako msituni akaonekana kuwa karibu sana na TAFF na baada ya muda mchache tukaona mikutano ya maridhiano baina ya TAFF na Bongo Movie na kwa kiasi fulani ikawa inaonekana kama TAFF imepoteza mwelekeo, haikuwa na inapoangalia. Nilijikuta nikifurahia igizo lilivyokuwa likiendelea.

Baada ya ujio wa katibu mpya naona zimeanza pilika za sera na muundo wa tasnia, nautakia heri umoja katika tasnia ya filamu ila wenye dhamana waendelee kuuhubiri na kuupigania. Kwa sisi wengine ngoja tufanye mengine, kama yatasaidia katika kuleta umoja ndiyo furaha yetu sote.
Nawasilisha.

Like our Facebook page Swahili World Planet for more updates about Tanzanian movie stars' latest gossips, news, fashions, music plus Hollywood, Bollywood and Nollywood news.

No comments:

Post a Comment