Wednesday, September 18, 2013

TUPIGANIE BODI HURU YA FILAMU ILI KUONGEZA UFANISI: BISHOP HILUKA

Soma andishi hili lenye hoja nzuri za kuijenga  tasnia ya filamu Tanzania kutoka kwa mwanaharakati wa tasnia ya filamu nchini ndugu Bishop Hiluka ambaye pia ni mmoja wa viongozi wa Shirikisho la filamu Tanzania(TAFF)..................

"Ili kuongeza ufanisi: tupiganie Bodi Huru ya Filamu"

 Kama wadau wa filamu tufikirie kutumia Maonesho ya Biashara ya Kimataifa kama haya ya Dar es Salaam ambayo ni njia nzuri sana katika kujitangaza kitaifa na kimataifa


INASEMWA kuwa sekta ya filamu nchini kwa sasa imerasimishwa, jambo ambalo limekuwa haliniingii akilini kwa kuwa sijaona mfumo wowote unaotuashiria kwamba sasa tuko rasmi zaidi ya huu wa kulipa kodi kupitia stika za TRA. Hivi tumerasimishwa kwa Sera ipi hasa?
Sera ni hati muhimu inayoelezea thamani na kutokosekana kwa miongozo ya lazima na visheni. Nimewahi kuandika kabla kuwa bila sera madhubuti ya filamu maendeleo katika sekta hii yatabaki kuwa ndoto hata kama viongozi wa serikali watatuahidi mambo makubwa kiasi gani. Lakini kwanini tuendelee kuongozwa kwa matamko ya viongozi badala ya kupigania uwepo wa sheria?
Tarehe 9 na 10 mwezi huu tulikuwa na kongamano la kitaifa la wadau wa filamu kuhusu mapendekezo ya Sera ya Filamu itakayotuongoza katika sekta ya filamu ili tufikie mafanikio. Katika kongamano hilo lililoandaliwa na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) mambo mengi yalijadiliwa, lakini leo ningependa kujikita kwenye jambo moja: Bodi ya Filamu (Tanzania Film Board).
Bodi hii ya Filamu ni tofauti na Bodi ya Ukaguzi wa Filamu (Tanzania Film Censorship Board) iliyopo iliyoundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 4 ya 1976, hii ninayoikusudia ni Bodi Huru ya Filamu itakayowezeshwa na serikali (an independent government supported board) ikiwa na idara kadhaa zinazoshughulikia masuala ya filamu ili kupunguza mlolongo wa taratibu ambazo zimekuwa chini ya sheria na mamlaka mbalimbali (one stop shop).
Hapa pana tofauti kubwa kati ya Bodi ya Ukaguzi wa Filamu tuliyoizoea na Bodi ya Filamu ninayoikusudia (Independent Film Board), tofauti hiyo ni katika muundo na majukumu yake. Bodi ya Ukaguzi wa Filamu iliyopo ni chombo cha Serikali na ina majukumu makubwa ya kukagua na kupanga madaraja ya filamu na michezo ya kuigiza; kukagua na kutoa vibali kwa maeneo yote yanayotumika kwa maonesho na usambazaji wa filamu au michezo ya kuigiza; kuafiki na kutoa vibali kwa shughuli za usambazaji wa filamu na michezo ya kuigiza; kuafiki na kutoa vibali kwa maonesho ya filamu na michezo ya kuigiza. Pia kuafiki, kuzuia au kudhibiti maonesho na usambazaji wa filamu na michezo ya kuigiza.
Bodi hii ya ukaguzi imerithi sheria zilezile za kibaguzi za mkoloni (censorship laws) zilizotumika kukagua sinema na kuondoa baadhi ya vipande visivyotakiwa kutazamwa na Waafrika. Yaani tulikuwa tunapangiwa nini cha kutazama na nini hatupaswi tutazame. Lakini kwa mazingira ya sasa, sisi wote ni Watanzania, tunaujua utamaduni wetu na tunafanya sinema za Kitanzania kwa ajili ya Watanzania, kwanini tuwe na chombo cha kutukagua, kutupangia na kutueleza kipi ni cha Kitanzania na kipi si cha Kitanzania?

Soma zaidi hapa TUPIGANIE BODI HURU YA FILAMU ILI KUONGEZA UFANISI.



Follow us on twitter Swahili World Planet  and Like our facebook pages Swahili World Planet and Bongomovies SWP for more updates about Swahili movies latest news, gossip, celebrities, features, beauty, fashions, music plus Hollywood, Bollywood and Nollywood news.

No comments:

Post a Comment