Tuesday, June 11, 2013

WARAKA WA MATUKIO CHUMA, USOME HAPA


WARAKA WANGU
Nawasalimu kutoka katika ardhi jadidu ya mrefu ukaitwa mlima Kilimanjaro, nikipigwa upepo murua unukiao marashi yakaitwa karafuu, visiwa Unguja nayo Pemba kutengeneza Zanzibar, alipoishi binadamu akawa wa Kwanza, Ngorongoro kati ya vingi vya kujivunia na fahari kuitikia.
Labda tumekuwa tukisikia neno Kioo cha Jamii, na ama baada tukawa tunapeleka fikra zetu moja kwa moja kwa wale maarufu tunaowaona, kuwasikia ama kuwashabikia, iwe katika Nyanja ya sanaa, burudani, siasa, biashara, teknolojia na mengineyo kadha wa kadha. Lakini je tumewahi kuwaza kuwa Kioo cha Jamii ni kila mmoja wetu kwa nafasi yake, iwapo hutajiheshimu na kuiheshimu jamii uliyopo, kuanzia nyumbani, jirani, shuleni, kazini, chuoni, ibadani ama kwingine popote ulipo, wale wakutizamao watawezaje kukua na kuweza kuwa Kioo cha Jamii kile unachotaka wewe kukiona ama ikiwa hata kwako hukuwahi kukitanabahi?

Ujana – Maji Ya Moto
Umeshawahi kuusikia msemo huu, umewahi kukaa chini na kutafakari maana yake na kisha umuhimu wake? Wale tuwaonao leo na kuwakebehi, kuwadhihaki na labda kuwacheka kama si kuwadhalilisha kwa kufikia walipofikia pasipo labda mafanikio ama walichostahili kwa ukubwa leo umri wao, ushawahi kutambua kuwa nao waliwahi kuwa vijana, damu zikichemka, mihemko ikihemka na yaliyomo na yasiyomo kujitwisha na kabla hawajatanabahi jua likazimika na giza kuingia likawafika?

Umaarufu, Jeuri, Makidai na Maisha Yetu
Ushawahi kusikia mtoto akisema nataka kuwa maarufu akiwa mkubwa? Si kosa wala si vibaya, lakini swali kubwa unataka kuwa Maarufu kwa sababu gani, ili iweje na kwanini? Ushawahi kusikia ujumbe wa wimbo ukisema chuo kikuu cha umaarufu bongo ni dharau, jeuri, kiburi na majigambo? Umewahi kujiuliza kama wewe ni mmojawapo wa wahanga wa chuo hicho ambacho wakati mwingine ni kigumu mno kuepukika wakati wa ujana na hasa Umaarufu ama Mafanikio yanapokuja katika umri mdogo? 

Maisha YETU, CHAGUO LETU
Maisha ni uchaguzi na labda huwezi kuchagua uzaliwe katika hali ipi ya kipato, makazi ama ndugu na wazazi, lakini kwa hakika Hatima zetu tunapokuwa na kuwa na maamuzi yetu, NI UCHAGUZI WETU. Ushawahi kufikiri ni wangapi wanaoishi kwa maisha ya kuigiza alimradi waonekane wapo juu, wana fedha nyingi ama mafanikio mengi sana (hata kama mengine bado ni ndoto wanazoota), wajitutumuao kukidhi starehe, matumizi na manunuzi yasiyo na chembe ya uwekezaji bali ufujaji, huku bila kujua wakiendelea kujiongezea msongo wa mawazo, mateso, maisha yasiyo na hata chembe ya furaha ya kweli na mahangaiko yaliyojaa wingi wa makwazo na maigizo? Kuwa mmoja kati yao si lazima, ni CHAGUO LAKO, ni MAISHA YAKO.

KIPAJI / KIPAWA/ KARAMA vs TAALUMA, MALENGO NA USIMAMIZI
Labda mara nyingi kumekuwa na kuchanganywa kati ya mtu kuwa na kipaji, kipawa ama karama fulani ikiwezekana hata zaidi ya moja na kusahau umuhimu wa taaluma, malengo na uongozi na usimamizi ili kuweza kuchochea, kulinda na kustawisha mafanikio na uendelevu wa kilichopo kipaji, kipawa ama karama.  Si lazima mtu awe amesoma sana ili afanikiwe na vilevile kusoma haimaanishi moja kwa moja ni lazima ufanikiwe, katika kila jambo tunahitaji upambanuzi yakinifu, KUJITAMBUA, nia madhubuti, usimamizi ama uongozi sahihi na kubwa zaidi kutambua THAMANI YA UWEPO WETU na kuwainua wengine kupitia vipawa, uwezo, mafanikio ama mamlaka yetu.

Uwiano kati ya NAFSI na MIILI yetu
Umewahi kuwaza umuhimu wa uwiano kati ya nafsi yaani ile iliyopo ndani yetu na miili yetu yaani kile kila mwanadamu mwingine anachokiona kwa macho kwetu? Mara nyingi tumejikuta tukichanganya sana muonekano wetu mbele za watu, kwa maana ya miili, mavazi, mapambo, mali n.k na kusahau kabisa Nafsi zilizopo ndani yetu, na mwisho wa siku kukosa mawasiliano wala uwiano na kabla hatujajua kutumbukia kwenye matumizi mabaya ya vilevi, madawa, vitu vya kutuchangamsha ama kutuondolea na aibu na kuendelea kutopea kwenye dimbwi la furaha isiyo halisi na kusahau nafsi zilizo ndani yetu kabala hatujajua tukikimbilia umauti badala ya kuishi, ushawahi kutathmini umuhimu wa imani, dini, ushauri na maisha yenye malengo katika kulisha sio tu mwili bali pia nafsi na roho zetu?

Umaarufu wa leo, kutumika kwa leo, KILIO CHA KESHO
Kwa nini ukubali kutumika kwa sababu tu ya fedha ama maslahi Fulani na kusahau utu, thamani na uendelezaji za tasnia zilizotuweka pale tulipo? Na kwanini tujisahau kiasi kuwa wale waliotufikisha pale tulipo leo hii tukawasabahi ama kuwajulia hali kwa kiburi, dharau, makidai na jeuri, wale tuliokuwa tukiwasihi watuunge mkono ili tusonge leo wakawa si kitu kwani wako wengi wanaotutambua na kutufahamu (Mwinyi mwenye KITU asie na kitu kinyama cha MWITU?)

SHUKRANI
Kwa kila tukifanyacho, tukumbuke kutoa shukrani kwa wale waliotusaidia kwa njia moja ama nyingine, HAITUPUNGUZII BALI INATUONGEZEA zaidi na zaidi, tusikubali kushukuru tu alimradi tumepewa ama kuahidiwa kitu Fulani bali tujifunze kutoa SHUKRANI kwa KILA ANAESTAHILI.

Matukio-Amani OleAfrika Aranyande M Chuma ukiniita Mwafrika kwa FAHARI NITAITIKA.

No comments:

Post a Comment