Tuesday, May 21, 2013

TATIZO NA SULUHISHO LA HADITHI NYINGI ZA FILAMU KUJIRUDIA SWAHILIWOOD.

Kumekuwa na tatizo kubwa la hadithi/story nyingi za baadhi ya filamu za Kitanzania kujirudia na hao waandishi wa story pia wanalijua hili lakini bado hawajui wafanye nini ila tatizo ni lao na wao ndiyo wa kulitatua. Takribani wiki mbili sasa nimejaribu kuwauliza waandishi 6 wa filamu za kiswahili kati yao 3 wana majina makubwa na watatu ni chipukizi. Kila mtu kwa muda wake wa upatikanaji nilimuuliza hivi "ndani ya mwezi huu umeangalia filamu ngapi mpya za waandishi wengine wa filamu?", "katika miezi 3 iliyopita umeangalia filamu ngapi mpya na za zamani za waandishi wenzako?". Majibu ya watu 5 yalikuwa yanasema kuwa hawana muda wa kutosha kuangalia filamu za wengine kwa kuwa wapo busy sana na mambo ya filamu zao na mambo yao binafsi nje ya filamu hivyo kwa mwezi anaweza kuangalia kazi 2 au 1 ya mwandishi mwingine. Mwandishi wa 6 ambaye ana jina kidogo alisema huwa anaangalia za wengine kwa mwezi kama filamu 4 hivi. Mpaka hapo nikapata jibu kuwa waandishi wengi wa filamu za Kitanzania hawaangalii kazi za wenzao na ndiyo chanzo kikuu cha story kuingiliana sana kwakuwa kama mwandishi angekuwa anaangalia kazi mpya za wengine mara kwa mara na hata za zamani ni rahisi kuepuka idea ya story ambayo mwenzake kaitumia  tayari.

Tatizo hili la story kujirudia sana linaonekana pia katika filamu nyingi za Nigeria na na hata Ghana kwakuwa uzalishaji wa filamu ni mkubwa huku waandishi wakiwa hawaangalii kazi za wenzao kwa ukaribu, pia kutokuwepo kwa film critics ni tatizo moja wapo kwa kuwa hawa wangekuwa hawamkopeshi mwandishi au mtengeneza filamu ambaye hana jipya. Hollywood na Bollywood ukiziangalia kwa ukaribu ni kuwa waandishi wengi wanafuatilia kazi za wenzao licha ya kuwa wengi wao pia wamesomea taaluma husika na filamu kwa ujumla na hili unaligundua kwa urahisi ukisoma interviews zao mara kwa mara au filamu mpya inapoanza kutangzwa. Ni kweli kuwa wenzetu hawa wamepiga hatua kubwa kwa kuwa walianza zamani sana lakini na sisi tuanze sasa ili kufika walipo. Tatizo la kukopi kazi za wengine ni dogo sana sio kama watu wanavyodai story nyingi zinafanana kwa tatizo lililoelezwa hapo juu kwa hadithi za filamu kugongana sokoni bila waandishi husika kutojua tangu mwanzoni.

 Mfano wiki iliyopita mwandishi mmoja aliniletea story yake ili nimshauri kama kuna kosa lakini aliponielezea tu kwa ufupi story ilivyo nikamuuliza kuwa je umeangalia filamu mpya ya marehemu Kanumba Love & Power akasema hapana, nikamwambia nipe hiyo story niisome baada ya kusoma nikagundua kuwa story inashabihiana sana na ya filamu ya Kanumba. Yeye akaniuliza hiyo filamu unayo hapo nikamwambia sina ila nenda pale atakupa baada ya kuangalia akasema ahsante nimejifunza kitu kupenda kuangalia kazi za wengine ili kuwa professional. Ushauri ni kuwa waandishi wa story za filamu na hata screenwriters wawe wanaangalia sana kazi za wenzao ili kuepuka kurudia story bila sababu za msingi huku pia tujitahidi tukasomee taaluma hii kwa wale ambao vyeti vyao vya kitaaluma vinawaruhusu na pia kujiongezea ujuzi kwa kujisomea wenyewe pia. Kitaalam filamu inaweza kurudiwa upya lakini kuna taratibu zake, filamu za aina hii zinaitwa Remake ambazo hutokana na filamu za zamani za film industry husika au ya nje.

Vicent Kigosi(Ray) muigizaji, mwandishi na muongozaji Swahiliwood.

No comments:

Post a Comment