Thursday, October 23, 2014

BASATA Kumvua Sitti Mtemvu Taji La Miss Tanzania 2014, Wizara Waandaa Kikao.

Sitti Mtemvu
Sakata la lililojitokeza la mrembo wa Taifa wa mwaka huu 'Redd's Miss Tanzania 2014', Sitti Mtemvu kudaiwa kudanganya umri, limeingia katika sura mpya baada ya Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) kueleza kuwa litamvua taji hilo endapo itabainika kweli alichakachua umri wake.

Katibu Mkuu wa Basata, Geoffrey Mwingereza, aliliambia NIPASHE jana kuwa baraza hilo linasubiri uchunguzi ukamilike na endapo watabaini kuna udanganyifu ulifanyika hawatakuwa na la kufanya zaidi ya kumvua taji.

Wakati Mwingereza akieleza hayo, viongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wanatarajia kukutana leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili sakata hilo la Sitti.

 Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, alisema serikali imesikia taarifa za mkanganyiko kuhusiana na mrembo huyo hivyo imeamua kuitisha kikao ili kuanza kulifanyia kazi.

Nkamia alisema kamwe serikali haiwezi kukaa kimya pale ambapo jina la nchi linatajwa vibaya.

"Siwezi kukuambia hatua gani zitachukuliwa, ila kesho (leo) tutakuwa na kikao, serikali haiwezi kukaa kimya, kuna vyombo vyake vinalifanyia kazi," alisema Naibu Waziri huyo.

Aliongeza kuwa yeye alikuwa nje ya Dar es Salaam, lakini tayari kuna maelekezo aliyoyatoa na yameanza kufanyiwa kazi na wizara hiyo.

Siku moja baada ya Sitti kutangazwa mshindi wa taji hilo, taarifa za mrembo huyo kuhusu umri wake zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha kuwa ana miaka 25, hivyo hana sifa za kushiriki shindano hilo hapa nchini.

Nakala ya hati ya kusafiria ya mrembo huyo ambayo ilitolewa Februari 15, 2007 na muda wake wa kumaliza kutumika ukiwa ni Februari 14, 2017 yenye namba AB 202696 inaonesha Sitti ambaye pia anashikilia taji la Kitongoji cha Chang'ombe na Kanda ya Temeke, alizaliwa Mei 31, 1989.Pia taarifa nyingine zinazoone sha mrembo huyo ana miaka 25 ni zilizokuwa kwenye Taasisi ya Explore Talent, ikimtaja kwamba anaishi Dallas, Texas, urefu wake ni 5'8, umbo lake ni la kati, asili yake ni Mwafrika na rangi ya macho yake ni kahawia.

Juzi, Kamati ya Miss Tanzania iliyoko chini ya Mratibu wa shindano hilo, Hashim Lundenga, ilisema kuwa Sitti amezaliwa Mei 31, 1991 katika wilaya ya Temeke jijini kwa mujibu wa cheti chake cha kuzaliwa alichokionesha.

Lundenga alionesha cheti cha kuzaliwa cha Sitti ambacho kimetolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Septemba 9, mwaka huu kikiwa na namba 1000580309 na kikimtaja baba yake ni Abbas Mtemvu Zuberi (Mbunge- Temeke) wakati mama ni Mariam Nassor Juma (Diwani- Temeke).

Hata hivyo, Lundenga alisema kuwa kamati yake inaendelea na uchunguzi kuhusiana na taarifa hizo na endapo watabaini kuwepo na udanganyifu watamchukulia hatua mrembo huyo kwa kushirikiana na Basata.

Pia Lundenga na Sitti, walikanusha taarifa za mrembo kuwa kuwa na mtoto na kusema kwamba mwenye uthibitisho wa jambo hilo anatakiwa aliwasilishe kwa kamati ili hatua zichukuliwe.

Sitti aliibuka kidedea katika shindano la urembo la taifa lililofanyika usiku wa Jumamosi ya Oktoba 11 kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini na kuwashinda washiriki wenzake 29 waliokuwa wanawania taji hilo.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment