Mrembo Sasha Juma, 20, kwa sasa anapitia kipindi cha majuto, analipia
gharama ya kujivalisha ubandidu na kujisingizia kupewa mimba na
supastaa, Nasibu Abdul Juma ‘Diamond’.
Sasha, akiwa na macho makavu, alitamka mbele ya waandishi wetu kuwa
mimba hiyo aliyopewa na Diamond, ilimgharimu kufukuzwa shule akiwa
kidato cha nne mwaka jana.
Unadhani Sasha analo tena? Ameshaumbuka na baada ya simulizi yake ya kutunga kushtukiwa, hivi sasa mrembo huyo anatishia kujiua.
Mr. Juma ambaye ni baba mzazi wa Sasha, aliliambia Risasi Mchanganyiko:
“Huyu mtoto ametishia kujiua, anajua makosa aliyoyafanya. Anataka
kutuvuruga vichwa, ukweli ni kwamba kila alichokisema kuhusu Diamond ni
uongo mtupu.
“Nahisi kuna mtu yupo nyuma yake, sasa anataka kumtumia ili kumchafua
Diamond, upande mwingine akili yangu inaniambia yule mtoto anataka
umaarufu, maana najua yule ni mwigizaji, sasa pengine anataka kutoka.”
UONGO WA SASHA
Risasi, lilipata taarifa kuhusu malalamiko ya Sasha ambaye alikuwa
akidai kupotezewa dira ya maisha na Diamond kwa sababu alimpa mimba na
kumtelekeza na mtoto mwenye umri wa miezi minne.
Baada ya kupata ‘tipu’ hiyo, mwandishi wetu alimsaka kwa udi na uvumba
mpaka Septemba 4, mwaka huu (Jumatano ya wiki iliyopita) ambapo mrembo
huyo alitia maguu kwenye mjengo mkubwa wa magazeti pendwa nchini
Tanzania.
Baada ya kuwasili makao makuu ya Global Publishers, Bamaga, Mwenge, Dar
es Salaam, Sasha aliingizwa kwenye chumba maalum chenye mitambo ya
kurekodi sauti na picha kisha akaanza kumwaga simulizi yake.
Alidai kuwa alikutana na Diamond, Mlimani City, mwaka jana, wakapeana
namba za simu kabla ya kuanzisha uhusiano wa kimapenzi ambao
uliwafikisha kwenye ‘kategori’ ya kuparamia kitandani na kutenda mchezo
wa baba na mama pasipo kutumia na kinga.
“Nilipopata mimba Diamond alinishawishi nisitoe, akaniahidi atanisomesha
hata kama nitafukuzwa shule. Baadaye nilifukuzwa shule, akazidi kunipa
moyo kwamba atanilinda. Mimba ilipokuwa kubwa akapotea, nilipozaa
hakujitokeza.
“Diamond akawa siyo yule ambaye alikuwa ananipa moyo. Alibadilika, hali
hiyo ikanifanya nione mwanangu hana baba, hata cheti za kuzaliwa,
sijamwandika Diamond, mtoto wangu nimempa ubini wa baba yangu, yaani ya
Juma.”
NI UONGO MTAKATIFU
Ili kukamilisha habari hiyo ambayo ilitoka kwenye gazeti hili, toleo la
Jumamosi iliyopita, mwandishi wetu aliwasiliana na baba mzazi wa Sasha
(Mr. Juma) ambaye alipoambiwa kuhusu mwanaye kuzaa na Diamond, alishtuka
kisha akasema:
“Unajua yule mtoto sikai naye, anaishi na mama yake. Mimi sijui chochote
ila nashangaa, inawezekanaje apate mimba mpaka azae mimi baba yake
sijui? Ngoja niongee na mama yake.”
Mr. Juma alipiga simu kuzungumza na mama yake Sasha mbele ya mwandishi wetu. Mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo;
MR. JUMA: Habari yako.
MAMA SASHA: Salama tu, za kwako?
MR. JUMA: Namshukuru Mungu, ebwana mbona Sasha kaongea na mwandishi wa habari anasema kapewa mimba na Diamond na amezaa?
MAMA SASHA: Wewe si unajua haya mambo ya vijana?
MR. JUMA: Mambo ya vijana kivipi? Ina maana mtoto anapata ujauzito mpaka anazaa wewe na baba yake hamjui?
MAMA SASHA: Baba nani, si wewe?
MR. JUMA: Mimi baba yake sijui, ndiyo maana nakuuliza wewe, maana nimesikia umekuwa unawasiliana na Diamond kuhusu hili.
MAMA SASHA: Nani kakwambia? Nimeshasema hayo ni mambo ya watoto, naomba umuulize mwanao vizuri, kama hauna namba yake nikutumie.
Katika mazungumzo hayo, Mama Sasha, hakumpa majibu ya moja kwa moja
mzazi mwenzake, kuhusu binti huyo kupata mimba, kuzaa na Diamond kuwa
mhusika.
RIPOTI YA WIKI HII
Mr. Juma alifika ofisi za Global Publishers na kueleza: “Jana (Jumapili
iliyopita), nilimchukua Sasha na kuzungumza naye kwa kirefu, kwa kifupi
alikiri kuwa hajawahi kupata mimba na yule mtoto si wa kwake.
“Mtoto imebainika ni wa dada yake, yaani mtoto mkubwa wa Mama Sasha
ambaye anaitwa Khadija. Kuna kitu cha kujifunza hapa kuwa Sasha
aliwadanganya mpaka watu ambao niliwakabidhi ili wamsaidie kisanii.
“Kabla sijaongea kwa kirefu na Sasha, nilizungumza na Thabit Abdul
(mwanamuziki wa Five Stars) ambaye nilimkabidhi kwake kumsimamia
kisanii, nikamuuliza inakuwaje mtoto anapata mimba? Akanijibu hata yeye
anashangaa. Kwani hata yeye alishangaa kumuona Sasha akiwa na picha
nyingi amebeba mtoto kwenye simu yake.
“Akamuuliza umezaa akajibu ndiyo. Hisia zangu zinazunguka katika mambo
mawili, ama aliamua kutunga ili kupata umaarufu kupitia jina la Diamond
au alitumwa na mtu. Jana wakati nazungumza na Sasha, nilikasirika sana,
nikaona hatutafika pazuri.
“Ikabidi nimpigie simu rafiki yangu mmoja ili amwite azungumze naye.
Kweli alimwita wakazungumza, baadaye yule rafiki yangu akaniambia Sasha
kasema anaona mambo yanazidi kuwa makubwa, kwa hiyo anataka kunywa sumu
afe. Namshangaa sana huyu mtoto, sijui ana kichaa gani?”
UKWELI NI HUU
Kwa mujibu uchunguzi wetu usio na shaka, mtoto aliyepigwa picha akiwa
amebebwa na Sasha, mama yake halisi ni dada wa mrembo huyo ambaye ni
Khadija.
Sasha na Khadija wanaunganishwa na mama yao lakini kila mmoja ana baba yake.
Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa kwa sasa Khadija anaishi na mwanaye mkoani
Tanga, huku Sasha akiendelea kupuyanga ndani ya Jiji la Dar, akiwa
hajui tamu wala chungu ya kunyonyesha, vilevile hajawahi kusikia uchungu
wa uzazi wala hatambui sura ya ‘leba’ ilivyo.
Khadija akizungumza kupitia simu ya Mr. Juma, huku mwandishi wetu
akifuatilia mazungumzo, alisema: “Nikija Dar nitafika Global, mimi ndiyo
mama wa yule mtoto na zile picha Sasha alipiga na mtoto siku ya
arobaini yake.
“Sasha anataka kunisababishia matatizo na baba mzazi wa mtoto. Mimi kama
mama mzazi wa mtoto, simjui Diamond, kwa hiyo hahusiki chochote na
mtoto wangu.”
Aidha, Mr. Juma alisema kuwa alimpigia simu Diamond na kumuweka sawa kuhusiana na tuhuma ambazo binti yake alimsakizia.
“Diamond anajua kila kitu, nimeshaongea naye na nimejaribu kumtaka
atulize munkari, maana ni wazi zile taarifa zimemchukiza sana. Kweli
zimemchukiza.”
DIAMOND ANASEMAJE?
Gazeti hili lilipozungumza na Diamond, alisema: “Nilishasema simjui huyo
Sasha, ahadi yangu ipo palepale, nitampeleka mahakamani. Amenichafua
sana.
“Masharti yangu ni haya, kama anataka nimsamehe aende kweye redio na televisheni akatangaze kwamba sijampa mimba.”
Aibu ambayo Sasha anakutana nayo sasa na tishio la kuburuzwa mahakamani
ambalo analikabili kutoka kwa Diamond ni onyo kwa watu wengine ambao
wamekuwa na tabia za kuwasingizia wenzao ili kujipatia umaarufu.
Taarifa ni kwamba tangu alipoumbuka, Sasha amekuwa mtu wa
kujificha, akikwepa kukutana na watu ambao wanajua mkanda mzima wa
simulizi yake ya kutunga.
source:globalpublishers
Follow us on twitter Swahili World Planet and Like our facebook pages Swahili World Planet and Bongomovies SWP
for more updates about Swahili movies latest news, gossip, celebrities,
features, beauty, fashions, music plus Hollywood, Bollywood and
Nollywood new
No comments:
Post a Comment