Muigizaji huyo maarufu na wa siku nyingi nchini ambaye pia ni producer, director na sasa anasambaza kazi zake mwenyewe ameandika "BILA STEPS INAWEZEKANA
Kwa muda mrefu nimekuwa nikiulizwa sababu ya kuamua kusambaza filamu
zangu mwenyewe badala ya kuzipeleka kwa wasambazaji ambao nilikuwa
nikifanya nao kazi kwa muda mrefu, yaani kampuni ya Steps Entertainment.
Najua maswali yamekuwa mengi kwa kuwa kuna watayarishaji
wengi wa filamu nchini wanaohangaika usiku na mchana ili kupata mkataba
wa kufanya kazi chini ya kampuni hiyo kwa kuwa Steps Entertainment ndiyo
kampuni ya usambazaji inayolipa vizuri zaidi kuliko makampuni mengine
yote kwa sasa.
Leo nimeamua kuongea walau kidogo …….
“Kwanza nikiri kuwa maneno ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania,
mhesimiwa Dr. Jakaya Kikwete aliyotamka siku aliyoiita Ikulu kamati ya
mazishi ya marehemu Steven Kanumba ndiyo yamekuwa yakinisukuma sana hadi
kufikia uamuzi huu mzito.
Kati ya waliounda kamati hiyo
iliyoitwa Ikulu, mimi nilikuwa katibu, Mwenyekiti alikuwa Gabriel Mtitu
au maarufu kama Mtitu Game, pia kulikuwa na wajumbe wengine kama Ruge
Mutahaba, Asha Baraka, Jacob Steven ‘JB’ na Mzee Chilo. Baada ya kuongea
mengi kuhusiana na msiba wa Kanumba na mazishi yake, mheshimiwa rais
aliuliza ‘Hivi marehemu Kanumba kaacha filamu ngapi?”
Kwa aibu
tulimjibu mheshimiwa rais kuwa marehemu Kanumba hajaacha hata filamu
moja, zote ni za msambazaji wake na hata mbili ambazo zilikuwa
hazijatoka yaani ‘Ndoa yangu’ na ‘Love & Power’ tayari zilikuwa ni
za msambazaji kutokana na aina ya mkataba tunayoingia na msambazaji.
Mheshimiwa Rais alisikitika sana, akatuambia kuwa yeye hawezi kutumia
nguvu kutukataza kuuza mali zetu lakini angependa kuona kuwa tunamiliki
wenyewe filamu zetu na tutakapoona tumekwama tumwambie. Aliongeza kuwa
kuuza haki zetu ni kama kuuza utu wetu. Maneno ya mheshimiwa Rais
yalinichoma sana.
Mimi ni msanii wa kwanza kufanya kazi na
kampuni hiyo kama mtayarishaji wa filamu na filamu yao ya kwanza
kuisambaza ilikuwa ni ‘Jeraha la Ndoa’ ambayo niliitengeneza mimi. Na
kwa kuthibitisha hilo, mwaka huu kampuni hiyo ya Steps ilitoa tuzo ya
heshima kwa kampuni yangu ya 5 Effects Movies Ltd kwa ajili hiyo.
Nasikitika kukiri kuwa filamu zote ambazo nilizitengeneza kisha
zikasambazwa na kampuni ya Steps, siyo zangu tena. Kampuni hiyo imekuwa
ikinunua haki zote za filamu wanazopelekewa kwa ajili ya kuzisambaza kwa
hiyo baada tu ya kusaini mkataba wao unakuwa huwezi kufaidika tena na
chochote kutokana na mauzo au faida nyingine zinazotokana na filamu
yako.
Kwa aina ya mikataba ambayo wasanii na watayarishaji
tunaingia na kampuni ya Steps Entertainment, sisi tumekuwa ni wasimamizi
tu wafilamu za zao, yaani ni kama manyapara kwenye mashamba ya mkonge
wakati kwa ukoloni. Ni waajiriwa tusio na mafao ya uzeeni.
Kwa
taarifa tu ni kwamba filamu zote mnazoziona mitaani zikisambazwa na
kampuni siyo za hayo makampuni yanayotajwa kutengeneza filamu hizo bali
ni filamu za Steps Entertainment. Ndiyo maana hata ukienda kwenye Chama
cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) utakuta wasanii wakubwa hawamiliki
kabisa filamu lakini kampuni ya Steps inamiliki filamu zaidi ya 400.
Kifupi ni kuwa hadithi ni zetu, sehemu za kuigizia ni zetu, tunaigiza
sisi, tunarekodi na kuhariri sisi lakini filamu ni za Steps
Entertainment na ndiyo maana hata kampuni ya marehemu Steven Kanumba
‘Kanumba the Great’ imesambaratika baada ya kifo chake na mama yake
akikabiliana na ugumu wa maisha lakini filamu za Kanumba bado zinatesa
kwenye soko la filamu ndani na nje ya nchi.
Nawashangaa watu
wanaomshutumu mama mzazi wa Kanumba kuwa amemaliza mali za mwanae na
sasa anaishi kwa kufadhiliwa na Lulu, wangejua kilicho nyuma ya pazia
wangemuonea huruma badala ya kumshutumu. Wakati Steps wanakiri kuwa
filamu iliyowahi kuuza sana katika historia ya kampuni yao ni ‘Ndoa
yangu’ ya Kanumba, hawasemi kuwa familia yake imenufaika vipi zaidi ya
kupewa tuzo.
Pamoja na kununua haki zote za filamu, kampuni ya
Steps hawatoi malipo ya filamu wanazozinunua kwa muda muafaka hivyo
kutufanya tuendelee kuwa mafukara siku hadi siku. Hii ni sababu ya pili
ya mimi kujitoa Steps, sitaki familia yangu ije kudhalilika baada ya
kifo changu.
Fikiria unapeleka filamu yako Steps, mnaingia
mkataba wa kuuziana, lakini hawakulipi mpaka wakati watakapoamua
kuiingiza sokoni hivyo hata wakikaa mwaka bila kuiingiza utakaa mwaka
mzima unasuburi pesa. Hivi kweli mwaka huo utakuwa unakula nini kama
umeamua kuifanya sanaa kuwa kazi yako?
Cha kuchekesha hata
wanapoamua kuiingiza sokoni hawakulipi mpaka baada ya wiki mbili au tatu
baada ya filamu yako kuwa imeingia sokoni, utasema hapo wamekulipa au
umejilipa mwenyewe baada ya kuwa imenunuliwa?
Mfano mwingine
hai ni wa marehemu Said Juma Kilowoko (Sajuki) ambaye ni miongoni mwa
wasanii maarufu na watayarishaji wa filamu. Marehemu Sajuki alilazimika
kuzunguka na wasanii wenziye mikoani akiwa anamuwa taabani ili tu aweze
kupata fedha za matibabu jambo ambalo naamini lilimzidishia matatizo ya
kiafya.
Na kutokana na kuuza haki zetu zote ilibidi mkewe
Sajuki, Wastara atengeneze ‘Mr & Mrs Sajuki’ ili aweze kupata fedha
za kujikimu na kurekebisha mambo mbalimbali yaliyovurugika wakati
akimuuguza mumewe. Kama tungekuwa hatulazimiki kuuza haki zetu zote,
familia hiyo ingeweza japo kupeleka filamu zake kwenye vituo vya runinga
barani Afrika ambako ni chanzo kingine cha mapato kwa msanii.
Baada ya kutafakari kwa kina niliamua kulipia leseni ya usambazaji wa
filamu kupitia kampuni yangu ya 5 Effects Movies Ltd ili niwe nasambaza
filamu zangu nikitegemewa kupata sapoti kubwa kutoka kwa wasanii
wenzangu hasa mastaa wakubwa lakini imekuwa kinyume chake. Kwa sasa
naonekana adui mbele ya wenzangu.
Kupitia kampuni yangu ya 5
Effects Movies Ltd, niliingiza sokoni filamu ya ‘Omega the Confusion’,
na ndani ya masaa matano ya kwanza nilifanikiwa kurudisha gharama zangu
zote na kupata faida kidogo. Toka hapo hadi sasa inaendelea kukimbia
sokoni hivyo natengeneza faida tu na bado filamu ni yangu, naweza
kuifanyia chochote kama kuipeleka kwenye runinga za kimataifa n.k
Nimalizie kwa kuweka wazi kuwa sina ugomvi wowote na kampuni ya Steps,
mmiliki wake wala mtumishi yeyote wa kampuni hiyo. Pia sina chuki na
yeyote kati ya wanaoendelea kufanya kazi chini ya kampuni hiyo. Kikubwa
ni kuwa haya ni maisha na kila mmoja ana mtazamo wake katika kuyakabili
na kujiletea mafanikio”.
“WOGA WAKO NDIO UMASKINI WAKO” ‘TEAM NYATI’"
Follow us on twitter Swahili World Planet and Like our facebook pagesSwahili World Planet andBongomovies SWP
for more updates about Swahili movies latest news, gossip, celebrities,
features, beauty, fashions, music plus Hollywood, Bollywood and
Nollywood news.
No comments:
Post a Comment