Friday, October 24, 2014

Jihan Afungukia Ushindi Wa Sitti Mtemvu, Asema Ni Mtanzania Halisi Mama Msukuma Baba Mlebanon.

Jihan
Ushindi wa Sitti Mtemvu umekuwa gumzo katika tasnia ya urembo tangu atwae taji hilo kwa madai alipendelewa hakuwa na vigezo. Wengi wanadai Jihan Dimachk ndiye aliyestahili kushinda hivyo alionewa kuweka nafasi ya3.
Globalpublishers kupitia gazeti la Ijumaa imefanya mahojiano na Jihan kama ifuatavyo.......
Ijumaa: Habari yako Jihan, sisi ni waandishi kutoka Gazeti la Ijumaa.

Jihan: Okey, nashukuru kuwafahamu, karibuni.

Ijumaa: Tuanze na matokeo ya kinyang’anyiro cha Miss Tanzania mwaka huu, unadhani wewe ulistahili kuchukua nafasi ya tatu na Sitti Mtemvu kuibuka kidedea?
Jihan: Siwezi kuongea sana jamani lakini kwa kifupi nilikuwa nikiamini nitashinda, niseme tu kwamba it was unfair but I can’t explain (haikuwa sawa ila siwezi kuelezea).
Ijumaa: Kwa nini unasema hivyo? hebu fafanua kauli yako.
Jihan: Sipendi kuwa muongeaji sana, naheshimu maamuzi ya majaji na Kamati ya Miss Tanzania lakini ukweli uliopo moyoni mwangu ni kwamba nilijiamini na ndiyo maana niliingia kwenye kinyang’anyiro nikijua ushindi ni haki yangu.
Ijumaa: Wapo wanaosema ulikuwa na kila kigezo cha kuwa Miss Tanzania 2014 lakini umetoswa kutokana na rangi yako ukihisiwa wewe si Mtanzania, unaliongeleaje hili?

Jihan: Sipendi kabisa kusikia maneno hayo, mimi ni Mtanzania, nimezaliwa Mwanza, mama yangu ni Msukuma na baba yangu Mlebanon. Tangu naingia kwenye shindano hili waandaaji walinihoji, wakafuatilia hilo na kutambua ni Mtanzania, ingekuwa tofauti sidhani kama ningeruhusiwa kushiriki.

 Ijumaa: Kwa mfano ikitokea Sitti akavuliwa taji kutokana na haya yanayozungumzwa, uko tayari uvishwe wewe?
Jihan: Siwezi kulijibu swali hilo kwani haijatokea. Endapo itatokea na waandaaji wakanifuata kuniambia hivyo, hapo ndiyo nitakuwa na la kuzungumza.

Ijumaa: Unamuongeleaje Sitti Mtemvu?

Jihan: Kwa sababu ndiye aliyevishwa taji, naheshimu ushindi wake, namkubali kuwa ni mrembo na siwezi kupingana na maamuzi yaliyotolewa.
Ijumaa: Umechukua nafasi ya tatu ambayo nayo si haba, una mipango gani ya baadaye?

Jihan: Nina mambo mengi ya kufanya. Nina ndoto za kuwasaidia wanawake na watoto lakini pia nahisi nina jukumu la kusaidia katika suala la elimu nchini, nitajipanga kufanikisha hayo.

Ijumaa: Kwa nini elimu?
Jihan: Nimekuwa nikikutana na watu wengi ambao elimu imekuwa kikwazo kwenye maisha yao, nikawa nimejiapiza kuhakikisha nawasaidia kadiri nitakavyoweza.

Ijumaa: Asante sana Jihan, tunakutakia mafanikio katika yale unayopanga kuyafanya.

 Jihan: Nashukuru sana.

No comments:

Post a Comment