marehemu George Tyson |
Imeandikwa na Sultani Tamba
FILAMU ya Girlfriend iliyotengenezwa mwaka 2003, ambayo wadau wote wanakubaliana kwamba ndiyo iliyolipua moto wa watengeneza sinema wa Kitanzania, inabaki kuwa ndiyo filamu iliyomuweka rasmi George Otieno Okumu ‘Tyson’ kwenye ramani ya filamu za Tanzania na kumpa heshima kubwa.
George Tyson, Mkenya aliyekuwa akifanya shughuli zake hapa nchini alifariki dunia wiki iliyopita kwa ajali ya gari iliyotokea Morogoro alipokuwa akirejea Dar akitokea Dodoma.
Msiba huu mkubwa, umesikitisha wengi, hasa wadau wa filamu wanaporejea historia ya chachu ya filamu za Kibongo. Ni jambo lisilopingika kwamba Tyson alitusaidia kujenga misingi ya ajira kupitia filamu kutokana na mchango wake mkubwa.
Tangu mwaka tuliotengeneza filamu ile, 2003 hadi Tyson alipofariki dunia ni miaka 11 imepita. Matunda yake yangali yanaendelea kwa sababu moto ule uliowashwa, haujawahi kuzimika hadi leo, hamasa zilivyowajaa watengeneza filamu zingali zinaendelea na sasa tasnia hii imepanuka na imesaidia kutoa ajira kwa wengi.
Nafikiri ni wakati muafaka sasa wa mimi kuandika machache kuhusu filamu ile, nikikazia mchango kwa mtengeneza filamu marehemu George Tyson na kueleza mengine ambayo ni muhimu sana leo yakajulikana ili kuweka kumbukumbu juu ya filamu hii ya kihistoria.
Wazo la filamu ya Girlfriend lilikuwa ni la kwangu na lilitokana na makala yangu mwenyewe ambayo ilichapishwa kwenye gazeti tumbo moja na hili la Amani (nilikuwa mhariri kiongozi wa gazeti hilo kipindi hicho) iliyokuwa na kichwa cha habari kilichosema:
HIVI WASANII WA RUNINGA HAWANA WIVU AU UBUNIFU WA MAENDELEO YAO? Ilichapishwa kwenye toleo namba 216 la Novemba 14-20, 2002.
Kwa ufupi makala yenyewe ilihusu namna ambavyo sinema za Kinigeria zilivyokuwa zinapitishwa kuingia Bongo na kuuzwa kwa wingi huku wasanii wa nyumbani wakiwa hawaonekani kufanya juhudi zozote za kuonesha kwamba na wao wanaweza. Wakati ule michezo ya runinga ndiyo iliyokuwa ikitamba sana.
Niliichukua makala ile kama changamoto na ndipo nilipoandika hadithi ya filamu ambayo nililenga kuwahusisha wanamuziki wa Bongo Fleva ambao walikuwa juu kipindi hicho halafu wachanganyike na wale wa maigizo ya runinga. Lengo la kufanya hivyo lilikuwa ni kuinua sanaa ya filamu kupitia wasanii wa Bongo Fleva! Wazo hilo nilishirikiana na mwenzangu, Kessa Mwambeleko.
Lakini mimi sikuwa na ujuzi wowote kuhusu mambo ya filamu, japo nilikuwa ni mchambuzi wa maigizo magazetini, lakini sikuwahi kusoma wala kujua hasa filamu zinavyotengenezwa ndipo tulipokubaliana kumfuata George Tyson. Wakati huo alikuwa ameshaacha kazi ITV na alikuwa akiongoza Kikundi cha Nyota Academia kilichokuwa kikipatikana kwenye jumba la utamaduni wa watu wa Urusi.
Mwanzoni tulikuwa na mzuka wa kuhakikisha kazi hiyo inafanyika lakini hatukuwa na fedha! Mimi na mwenzangu tulijipa moyo kwamba fedha tutazipata tu, la msingi maandalizi kwa ajili ya filamu hiyo yaanze. Wakati huo hata jina la filamu sikuwa nalo, nilikuwa na hadithi tu mkononi.
Tulikubaliana na mwenzangu kwamba mimi ndiye nikamvae George Tyson ambaye kwa bahati tayari alikuwa ni rafiki yangu na kumweleza mpango wetu.
Tulikubaliana na mwenzangu kwamba mimi ndiye nikamvae George Tyson ambaye kwa bahati tayari alikuwa ni rafiki yangu na kumweleza mpango wetu.
Siku ya pili nilitoroka kazini, nikaenda ‘Russian Culture Centre’ na kukutana na George Tyson. Alinipokea kwa bashasha zote, nikamweleza kwa kina tunachotaka kufanya na hapohapo nikamkabidhi hadithi yenyewe na majina ya wasanii wa Bongo Fleva ambao tulipanga kuwatumia! Kuna mambo mawili nikamhakikishia.
La kwanza nilimwambia kwamba magazeti yote ya kampuni tunayofanyia kazi ya Global Publishers yataitangaza filamu hiyo kwa nguvu zote maana wafanyakazi wenzetu wote walifurahishwa na wazo letu na walikuwa tayari kusaidiana na sisi kwenye jambo hilo.
Jambo la pili, nilimwambia kwamba wasanii wote wa Bongo Fleva watakaoshiriki ni lazima warekodi wimbo ambao utakuwa ukipigwa kwenye vituo vya redio kuwamba ndiyo ‘soundtrack’ ya filamu ile.
Tyson si kwamba alikubali kwa moyo mmoja kuwa muongozaji wa filamu hiyo, lakini pia alipandwa na mzuka wa ajabu. Akanipa moyo kwamba filamu hiyo itatengenezwa na wasanii wote tuliowaandika watapatikana! La muhimu ni kwamba sisi tuingie ‘msituni’ kutafuta pesa za kuanza kuwalipa wasanii ‘advance!’
Hapo ndipo palipokuwa na kasheshe!
Kuanzia hapo, vikao baina yetu na Tyson vikawa ni kila siku, nyumbani kwake Kinondoni-Shamba, Dar na kwenye Mgahawa wa Best Bite Namanga.
Kuanzia hapo, vikao baina yetu na Tyson vikawa ni kila siku, nyumbani kwake Kinondoni-Shamba, Dar na kwenye Mgahawa wa Best Bite Namanga.
Hadi leo mimi na Yvone-Chery (Ngatikwa) ‘Monalisa’ ambaye alikuwa mke wa George Tyson kipindi hicho, tungali tunabishana kwamba jina la filamu ‘Girfriend’ alilitoa nani kati yangu mimi na yeye! Ila tunakubaliana kwamba ilikuwa ni usiku mmoja ambapo nilikula chakula cha usiku nyumbani kwao ndipo jina hilo likapatikana!
Kwa bahati nzuri, wasanii wote wa muziki tuliowaandika ambao ni King Crazy GK, AY, Jay Mo na TID, wote walikubali na mara moja walianza mazoezi kwenye ukumbi huohuo wa Russian Culture! Halafu Monalisa, Nina na wengineo ambao walikuwa wakitamba kwenye runinga kipindi hicho, nao wakajiunga nasi. Hiyo ilikuwa ni faraja kubwa kwetu, mimi na mwenzangu ambao tulikuwa tunahaha kutafuta pesa. Moto tuliouchokoza, ulikuwa unawaka!
George Tyson alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kushawishi, akalazimika kuwapiga ‘Kiswahili’ wasanii wale waendelee na mazoezi na wasubiri malipo yaliyochelewa kidogo!
Nakumbuka mmoja wa watu ambao walitusaidia ‘kutulindia’ heshima kwamba ‘pesa zipo’ alikuwa ni marehemu Mohamed Mpakanjia ‘Meddy’. Yeye tulimfuata na akakubali kuzungumza na wasanii na kuwatia moyo, yeye alikuja mazoezini kwa niaba ya Kepteni John Komba ambaye naye aliahidi kusaidia!
Wakati huo wote magazeti ya kampuni yetu na kampuni nyingine yalishaanza kuandika juu ya ujio wa filamu hiyo! Watu wakaanza kutafutana mjini!
Tyson aliendelea kuwa nguzo ya kazi ile, maana alifanikiwa kuwatuliza wasanii wote waendelee na mazoezi bila kujua kilichoendelea nyuma ya pazia.
Mungu si Athumani, kwa bahati nzuri tulipata pesa za malipo ya awali za wasanii kutoka kwa mfadhili mmoja ambaye alikubali kulipa! Hapo tukawa tumepiga hatua kubwa.
Tukawalipa wasanii wote pesa nusu za malipo yao na sasa ratiba ikasoma kwamba filamu itaanza kurekodiwa kwenye Ukumbi wa Club Bilicanas, wiki moja baadaye! Vurugu hizo zote tulizifanya kwa mwezi mmoja na wakati huo wote, mkurugenzi wa kampuni tunayofanyia kazi, Eric Shigongo alikuwa amesafiri Mwanza! Huku nyuma, meneja wetu, Abdallah Mrisho ‘Abby Cool’ tulikuwa tumemficha! Kiasi kwamba alikuwa hajui ‘movement’ zetu za kutokatoka ofisini zilihusiana na nini.
Wakati huo wote magazeti ya kampuni yetu na kampuni nyingine yalishaanza kuandika juu ya ujio wa filamu hiyo! Watu wakaanza kutafutana mjini!
Tyson aliendelea kuwa nguzo ya kazi ile, maana alifanikiwa kuwatuliza wasanii wote waendelee na mazoezi bila kujua kilichoendelea nyuma ya pazia.
Mungu si Athumani, kwa bahati nzuri tulipata pesa za malipo ya awali za wasanii kutoka kwa mfadhili mmoja ambaye alikubali kulipa! Hapo tukawa tumepiga hatua kubwa.
Tukawalipa wasanii wote pesa nusu za malipo yao na sasa ratiba ikasoma kwamba filamu itaanza kurekodiwa kwenye Ukumbi wa Club Bilicanas, wiki moja baadaye! Vurugu hizo zote tulizifanya kwa mwezi mmoja na wakati huo wote, mkurugenzi wa kampuni tunayofanyia kazi, Eric Shigongo alikuwa amesafiri Mwanza! Huku nyuma, meneja wetu, Abdallah Mrisho ‘Abby Cool’ tulikuwa tumemficha! Kiasi kwamba alikuwa hajui ‘movement’ zetu za kutokatoka ofisini zilihusiana na nini.
Na yeye tukamdanganya kwa kumsimulia kuhusu ujio wa filamu ya wasanii wa Bongo Fleva na sisi tukijifanya hatuijui! Akapendezwa sana na wazo hilo na kwenda Russian Culture, akapiga picha na kuja kupamba kwenye kurasa zake za katikati ambazo ni maarufu sana kwa burudani! Akawa amechangia kuanza kuitangaza! Siku chache baadaye, Shigongo akarudi!
Na yeye akasoma habari zilizoandikwa kwenye magazeti (yakiwemo yake mwenyewe) kuhusu ujio wa filamu ile! Akaipenda sana ‘aidia’ hiyo! Ila akawa hajui ni ya nani!
Kwa masikio yetu tukamsikia akisifia wazo hilo, mimi na mwenzangu tukatazamana!
Huo ulikuwa ni msala! Kwa jinsi bosi huyo alivyokuwa ‘siriaz’ na kazi, haingewezekana tena kuturuhusu ‘tutoketoke’ kwenda kufuatilia kuhusu filamu ile. Na mbaya zaidi, kesho yake ilikuwa ndiyo siku ya mkesha wa kuanza ‘shooting’ pale Club Bilicanas! Hadi hapo, hela ya kulipia ukumbi siku hiyo na gharama nyingine zote tulikuwa bado hatujapata!
Huo ulikuwa ni msala! Kwa jinsi bosi huyo alivyokuwa ‘siriaz’ na kazi, haingewezekana tena kuturuhusu ‘tutoketoke’ kwenda kufuatilia kuhusu filamu ile. Na mbaya zaidi, kesho yake ilikuwa ndiyo siku ya mkesha wa kuanza ‘shooting’ pale Club Bilicanas! Hadi hapo, hela ya kulipia ukumbi siku hiyo na gharama nyingine zote tulikuwa bado hatujapata!
Huku vichwa vikituuma tukakope wapi hela shooting ianze, huku bosi karudi. Hata kama tukijificha na kwenda ku-shoot, tayari atajua na akijua pengine filamu ingeishia hapo! Ndipo mimi na mwenzangu tukakaa kikao na kukubaliana kwamba tumwone meneja Abby Cool, tumtake ushauri! Kweli tukamfuata, akafurahishwa sana kugundua kwamba kumbe tulioanza kutikisa mji ni sisi wawili na wa tatu akiwa George Tyson. Akatushauri tumvae bosi tumweleze ukweli!
Katika tukio la kihistoria kabisa, Shigongo akalipokea wazo lile na tukamwomba tushirikiane naye kuitengeneza filamu hiyo! Amini usiamini papohapo baada ya kikao tu, Shigongo aliidhinisha kwa mhasibu tukachukue shilingi laki saba za kuanzia kazi Club Bilicanas kesho yake! Ilikuwa ni jambo la kusisimua sana!
Si tu alitoa pesa, Shigongo alihudhuria shooting yetu ya Bilicanas! Tulipata moyo sana!
Na hapa nataka niseme kitu ambacho watu wengi hawakuwa wakijua, filamu ya Girlfriend iligharamiwa kwa asilimia kubwa na Shigongo hadi ilipokamilika na kuzinduliwa kwa kishindo kikubwa ambacho haijapata kutokea kwa filamu yoyote nchini. Gharama nyingine ndogondogo kama mazoezi ya wasanii na malipo ya awali tulikopakopa kwa marafiki zetu! Kiasi tukawa tunanuka madeni!
Mimi na mwenzangu tulifanya juhudi kubwa kuwasiliana na Prodyuza wa Bongo Records, Paul Mathhyasse ‘P. Funk’ kufanikisha mpango wa kurekodi wimbo uliobeba filamu yenyewe. Japo tulipanga warekodi wasanii wote, lakini TID na Jay-Mo waliwahi kurekodi wimbo huo. Wasanii wenzao, King Crazy GK na AY walikuwa waungwana sana, waliridhika na wimbo ingawa hawakushiriki. Na hiyo ni kwa sababu ulikuwa ni wimbo mzuri sana.
Girfriend ilizinduliwa mara mbili jijini Dar, mara ya kwanza ni katika Hoteli ya Golden Tulip, Masaki ambapo hoteli ilifurika kupindukia kiasi kwamba kuanzia siku hiyo hoteli hiyo wakagoma kuruhusu uzinduzi wowote mwingine! Na mara ya pili yaani wiki moja baadaye filamu ilizinduliwa Diamond Jubilee na kujaza watu vilevile!
Kimsingi, Girlfriend isingefanikiwa kutengenezwa bila ya nguvu kazi, ujuzi na bidii kubwa sana iliyofanywa na marehemu George Tyson. Jinsi alivyonipa moyo mara ya kwanza nilipomfuata kisha yeye kuacha kazi zake zote na kushughulikia filamu hii, kilikuwa ni kitu cha kuvutia sana. Dairekta mwingine asingekubali kupoteza muda wake kufanya kazi ambayo hajui angelipwa vipi!
Mei 27, mwaka huu, nilimpigia simu ya kawaida George Tyson na kuongea mambo yetu ya kirafiki, jambo la ajabu ambalo lilinishangaza sana ni kwamba George Tyson alicheka sana kwenye simu siku hiyo. Kichekesho nilichomsimulia kilikuwa kidogo sana kulinganisha na kicheko alichotoa, alicheka mfululizo kiasi akaniambukiza na mimi nikacheka kama yeye.
Siku tatu baadaye nikapigiwa simu kwamba rafiki yako, George Tyson amefariki dunia kwa ajali ya gari.
Tangulia kaka, mchango wako hautasahaulika.
Tangulia kaka, mchango wako hautasahaulika.
Sultan Tamba ni mdau mkubwa wa burudani ambaye alifanya kazi kwa karibu na marehemu George Tyson.
source: Globalpublishers
Like our Facebook page Swahili World Planet for more updates about Tanzanian movie stars' latest gossips, news, fashions, music plus Hollywood, Bollywood and Nollywood news.
No comments:
Post a Comment