Daniel Manege ambaye ni producer, mwandishi wa miswada ya filamu na director wa filamu nchini aliendaka filamu kama vile Dereva Tax, Bado Natafuta, Shikamoo Mzee na nyinginezo ameshangazwa na Steps Kushusha bei ya filamu zake kwa kisingizio cha kupambana na uharamia. Manege amesema kuwa kitendo hicho sio kizuri hata kidogo kwa mustakabali wa tasnia ya filamu nchini. Soma andishi lake hapo chini.............
"Mimi kama mwandishi wa filamu na mtengeneza filamu nimesikitishwa na habari za kushushwa bei ya dvds za filamu mpaka sh.1000 ila ni jambo nililokuwa nikilitarajia litokee muda wowote kwani mfumo uliopo haumjengi msanii kukua kimaisha na pia kukuza kazi ya sanaa. Kwa muda mrefu nimekuwa mstari wa mbele kuwasihi wasanii na watengeneza filamu kwa ujumla kuweka fikra zao kwenye ubora zaidi, hilo ndilo suala la kwanza, msambazaji ni sehemu moja ya filamu, ubora wa filamu husika ni sehemu nyingine na soko ni sehemu inayojitegemea. Msambazaji wa filamu ni kiunganishi kati ya filamu na soko.
Kiunganishi hiki kina mchango mkubwa kukuza tasnia kama kikiangaliwa kwa umakini lakini pia si kiunganishi pekee, kuna aina nyingine nyingi za usambazaji. Aina ya usambazaji tunayotumia inaitwa "DISTRIBUTION 1.0" ambayo wenzetu waliacha kuitumia miaka ya 80 ambayo inasema, filamu inapokamilika basi msambazaji mmoja anapewa haki ya kuisambaza na kugawana mapato na producer. Ila baada ya kuingia aina tofauti za masoko kama Theatres "majumba ya filamu, Televisions, internet sasa kuna njia nyingi za kusambaza kazi za wasanii ukiachana na DVDs peke yake na aina hii ya usambazaji inaitwa "DISTRIBUTION 3.0", sasa msanii anapata mapato kwa kuonyesha filamu kwenye majumba ya cinema, kwenye mitandao, televisheni na festivals na hivyo kuwa na njia nyingi za mapato
Baada ya kutoa maelezo HAYO mafupi naomba nirudi kwenye mada yangu kuwa lazima kwanza tujali ubora wa kazi, tatizo lililopo ni kuwa hatuwezi kutoka kwenye mfumo dume wa DISTRIBUTION 1.0 ambao wenzetu wametoka tangu miaka ya 80 mpaka kufika DISRTIBUTION 3.0 kama kazi zetu hazitakuwa na ubora
Wengi watasema hatuna ubora sababu msambazaji anatulipa kidogo na tunashindwa kupata kipato cha kutengeneza filamu kubwa. Upande mmoja kweli ila upande mwingine si kweli kwani ukiandika Script iliyo bora na kutafuta makampuni ya kuweza kuifadhili na kuitetea script yako na kutumia muda kuangalia njia mbadala ya kutafuta masoko unaweza kupata pesa na kufanya filamu nzuri ambayo utaitumia kutengeneza jina na mauzo hata kama ni madogo ubora wa kazi hiyo utasaidia kukupa fursa nyingine na kugundua njia nyingine za masoko zikiwemo nilizoainisha hapo juu na support system itakayokusaidia kupata pesa za misaada (fund) zaidi.
Ndivyo Nigeria na Ghana wanavyofanya mpaka wanafika walipo na ndivyo pia Mimi nilivyofanya kuweza Kuproduce filamu yangu ya SAFARI YA GWALU (feature Salim Ahmed "Gabo" na Juma Rajabu "Cheche") ambayo watu wanaisubiri kwa hamu. Sijawahi kupeleka filamu kwa msambazaji ila Filamu nilizoandika kama DEREVA TAXI, NAKWENDA KWA MWANANGU, SHIKAMOO MZEE, BADO NATAFUTA na Script nzuri ya SAFARI YA GWALU Vimenisaidia kupata msaada wa fedha na naamini ubora wa SAFARI YA GWALU utasaidia kutengeneza njia mpya ya masoko.
Ninachoweza kusema kumalizia ni kuwa bado tuna mengi ya kujifunza kuhusu filamu, tujifunze kwa wenzetu na kutumia akili Mungu alizotupa kutafuta njia za kusaidia Tasnia hii yenye ushawishi mkubwa na yenye kuweza kututoa kwenye wimbi la ukosefu wa Ajira na kuliletea Taifa kipato na sifa kubwa. Msambazaji ni sehemu moja tu, Ubora wa Filamu utashawishi watu kuinunua filamu yako kwa gharama yoyote na kuitafuta popote ilipo hata nje ya nchi husika kwani " NGUVU YA USHAWISHI WA SANAA KWENYE MAISHA YA BINADAMU NI KUBWA KULIKO KITU CHOCHOTE KWANI SANAA NI LUGHA INAYOELEWEKA NA TAIFA, KABILA, DINI, ITIKADI NA JINSIA YOYOTE". Tusiwe waoga kujifunza na kujitoa kwa ajili ya mafanikio ya tasnia yetu. Tuungane kukuza tasnia yetu ya filamu. By Daniel Manege (Tanzanian Writer, Director and Producer)"
No comments:
Post a Comment