CAST: Issa Musa(Cloud 112), Wastara Juma, Jackson Kabirigi, Esha Buheti, Hidaya Njaidi.
DIRECTOR: Jackson Kabirigi, Cloud 112
RATING: 4/5
Cloud ni daktari anayefanya kazi mjini huku akiwa na maisha mazuri pamoja na mke wake Esha Buheti, hata hivyo Cloud anajihusisha na biashara zisizo halali. Siku moja mmoja wa watu wake katika kazi zake hizo anakuja akiwa na briefcase lenye madawa ya kulevya na kulibadilisha na jingine ofisini kwa Cloud ambalo halikuwa na madawa. Wakati Cloud anatoka kazini njiani anasimamishwa na askari ambao katika ukaguzi wao wanaona briefcase lenye madawa, Cloud anahukumiwa jela miaka mingi lakini mmoja wa watu wake wa karibu anamlipia faini na kutoka. Baada ya kutoka Cloud anakuwa hana mbele wala nyuma baada ya kufukuzwa kazi yake ya udaktari na mali zote kuchukuliwa. Anamfuata mmoja wa watu anaojuana nao amsaidie ambaye ana maisha mazuri ya hali ya juu huku mkewe akiwa ni Hidaya Njaidi, mtu yule anamshawishi Cloud aungane naye katika nguvu za giza ili kupata utajiri, Cloud bila kujua athari zake anakubali lakini mtoto wake na mtoto wa yule tajiri wanakufa ghafla baada ya ndumba kufanyika. Cloud anagombana na yule tajiri kwa kusababisha mwanae kufa huku msaada ukiwa hauonekani. Hatimaye Cloud anahamia kijijini mbali na watu huku maisha yake yakiwa yamebadilika akionekana mtu ambaye hata kisaikolojia ameathiriwa na hali iliyomkuta, huko anakutana na Wastara Juma na kufanikiwa kupata mtoto mwingine ambaye pia anakumbwa na mauzauza aliyowahi kufanya baba yake kipindi cha nyuma.
Kiukweli wakati naangalia filamu hii nilikuwa nasikia raha ya ajabu kuona kuwa Tanzania tunaanza kutengeneza filamu nzuri zenye viwango vya kimataifa, wakati naangalia filamu hii sikuona tofauti kubwa ya ubora na filamu nyingine nzuri za Afrika kama vile Nairobi Half Life. Filamu ni nzuri sana kuanzia story yake, hata mtu wa screenplay alijitahidi sana kufanya kazi nzuri ya kiwango cha juu, mtu huyo pia ndiye cameraman na editor wa filamu hii ambaye ni Timoth Conrad. Mtu wa mwanga pia alijitahidi kufanya kazi nzuri sana, costume na make up artist pia walitupa kazi nzuri.
Kwa upande wa performances waigizaji wote walijitahidi sana kukaa kwenye nafasi zao vizuri, Jackson kabirigi, Esha Buheti na Hidaya Njaidi walikuwa poa lakini ni Wastara Juma na Cloud ndiyo wanaokufanya upate hamasa zaidi ya kujua nini kitatokea katika filamu hii yenye kisa cha kusisimua mwanzo na mwisho huku katikati ikiwa kawaida. mwandishi alisuka vizuri kisa chake huku uteuzi wa location ukiendana na story husika.
Hata hivyo filamu hii iliharibiwa ubora wake mzuri wa kimataifa kwa kuwekwa katika sehemu mbili yaani part 1 & 2, sehemu ya kwanza ya filamu hii ni fupi sana, kwa ujumla ilitakiwa iwe sehemu moja tu na ingekuwa rahisi hata kutamba kwenye tuzo na film festivals za kimataifa. Tatizo hili linaoneka kusababishwa na kuchochewa na msambazaji wa filamu hii, wasambazaji wa filamu wanadaiwa kushupalia part 1 & 2 ambazo zinawanufaisha wao na sio wasanii huku wakishindwa kuweka kipaumbele katika ubora wa filamu kimataifa. Imefika hatua sasa wasambazaji muamke na kuacha kasumba hii inayozidi kuziweka filamu za Tanzania nyuma licha ya uwezo wa kufanya kazi kimataifa kuwepo. Irene Paul pia hivi karibuni alikaririwa akisema kuwa wasambazaji ndiyo tatizo kubwa la part 1 & 2 ambazo zinawanufaisha wao na sio wasanii. Jingne ni kuwa Cloud aliachana na mkewe wa kwanza Esha Buheti miaka kumi ilopita baada ya kugongwa na gari na kufa na baadaye kuzaa na Wastara lakini mtoto wa Wastara anaonekana kuwa kwenye miaka kumi au zaidi je Wastara na Cloud walikutanaje ghafla na kuzaa ndani ya miaka kumi na mtoto kuwa mkubwa si chini ya miaka kumi wakati Cloud alikuwa mtu ambaye kama kachanganyikiwa na maisha ! hata hivyo tatizo hili si rahisi mtu wa kawaida kuligundua haraka.
Kingine kinachosikitisha katika hii filamu ni kuwa watengenezaji wa filamu hii wanadaiwa kumnyima credit za uongozaji Jackson Kabirigi ambaye hata Wastata na Hidaya Njaidi walikiri kuwa Kabirigi ndiye aliyeiongoza kwa sehemu kubwa ila Cloud alisaidia mara chache sana hasa Kabirigi alipoigiza ila imeandikwa Cloud ndiye director huku Jackson kabirigi akijitoa katika kampuni ya Timamu Effects baada ya kutoakea tukio hilo. Inasikitisha mtu kushindwa kutambua mchango na uwezo mzuri wa mwenzake.
Kwa kumalizia ni kuwa ingawa filamu hii ilipoteza mvuto na ubora wake kwa kuwekwa katika part 1 & 2 lakini bado inastahili nominations kadhaa kwenye tuzo aidha za ndani au nje ya Tanzania katika Best Picture, Best actor(Cloud), Best actress(Wastara Juma), Best editing(Tomoth Conrad), Best director, Best make up, Best Costume, Best story, Best child artist, Best lighting. Itafute filamu hii uingalie kama bado hujaiona.
Cloud katika Dr.Max alikuwa na muonekano wa aina mbili uliovutia kwa namna moja au nyingine
Wastara licha ya kuwa na character ndogo katika Dr. Max lakini kipaji chake hakijifichi
No comments:
Post a Comment