Wednesday, May 1, 2013

KABLA YA BODI YA FILAMU KUPIGA MARUFUKU VIMINI KATIKA FILAMU NI MUHIMU KUITISHA MJADALA NA WADAU MUHIMU.

Kuna habari kuwa Serikali kupitia bodi ya filamu itapiga marufuku uvaaji wa mavazi yasiyo na maadili na vimini katika filamu za kitanzania hivi karibuni. Rais wa shirikisho la filamu Tanzania Simon Mwakifambwa amekiri pia hilo na kusema suala hilo pia litafanyiwa kazi na wizara ya habari, utamaduni na michezo. Hili ni wazo zuri lakini kuna shaka kidogo kama kweli wanaotaka kufanya hivi wameliangalia suala hili kwa undani au wanataka kufanya mambo juu juu tu kama baadhi ya mambo mengine huko nyuma kufanywa na watu wachache bila mjadala wa wadau mbali mbali na kutokuwa na mafanikio mazuri. Ikumbukwe kuwa huko nyuma filamu zinazoitwa zisizo na maadili zilizuiliwa lakini mpaka sasa hakuna mafanikio yoyote maana filamu zilezile zilizotolewa mfano kuwa kinyume na maadili zipo mpaka leo zinauzwa wazi wazi maeneo kama vile kariakoo, ubungo na kwingineko. Kingine ni kuwa nguo fupi katika filamu za kitanzania ni tatizo ambalo linaweza kutatuliwa kirahisi kuliko hata serikali kuingilia, tatizo ni kuwa hakuna watu wa mavazi katika filamu za kitanzania hivyo waigizaji wanajivalia tu nguo pasipo kuangalia maeneo husika muda na wakati lakini filamu inaweza kubuniwa mavazi mazuri tu yenye heshima na sehemu inayotaka hivyo vimini au hayo yanayoitwa yasiyo na heshima yakavaliwa katika sehemu husika na bila tatizo lolote na filamu ikawa nzuri.

Kama kweli serikali kupitia bodi ya filamu na wizara ya habari, utamaduni na michezo inataka kutafuta suluhu ya suala hili basi hao wenye mamlaka wasijiamulie wao wenyewe bila kuwashirikisha baadhi ya wataalam wa mavazi na watengenezaji wa filamu. Hii ni kwa sababu kila sehemu huwa na mavazi yake na filamu kuwa nzuri kimataifa ni lazima wahusika actors wawe wamevaa mavazi kulingana na scenes na maeneo husika na muda. Hata hivyo haimaanishi kuwa kuigiza kama changudoa ni lazima kuvaa mavazi mafupi lakini kuna sehemu ni lazima yahitajike. Hivyo mavazi hayo hayawezi kupigwa marufuku moja kwa moja kwa kuwa kuna baadhi ya story zinahitaji mavazi hayo katika baadhi ya scenes, na pia hata miaka ijayo baadhi ya watengeneza filamu wanaweza kushoot filamu zao hata ulaya kutokana na story zinavyotaka so baadhi ya mazingira ni vigumu kulazimisha hayo mavazi marefu na ya heshima. Bodi ya filamu na wizara zinatakiwa ziwaeleze watengeneza filamu kuhakikisha kuwa waigizaji wanavaa mavazi kulingana na story huku wakizingatia maadili pia.Huku wakianza kusisitiza kuwe na costume designers ambao ni rahisi kuwa makini na mavazi huku bado kukiwa na usasa kutokana na mahitaji ya scenes.

 Mfano india vazi la Bikini katika filamu liliruhusiwa tangu miaka ya 1960 lakini halivaliwi hovyo kwani huvaliwa kutokana na story na pia ni lazima actress awe na mwili wa kimisi unaoruhusu vazi hilo huku mwenyewe akiwa tayari kulivaa. Bikini siyo kuvaa nusu uchi kwa kuwa ni vazi lenye mazingira yake ambayo hayawezi kuingliana na vazi refu. Pia kama kweli serikali imeamua hivyo basi ipige marufuku filamu na video zote za wanamuziki kutoka nje ambazo huwaonyesha wakiwa nusu uchi au uchi zaidi kuliko wasanii wa Tanzania hapa italeta maana zaidi maana video hizo huonyeshwa mpaka kwenye television ya taifa. Huko nyuma kuna video ya mwanamuziki Q Chillah iliwahi kufungiwa kwa madai haina maadili lakini ilikua na afadhali kuliko za nje zinazoonyeshwa katika vituo vyetu. Kufanya hili itakuwa na maana zaidi na pia suala la mavazi mafupi katika filamu liangaliwe kutokana na mahitaji ya filamu na siyo kulichukulia juu juu tu ingawa ni kweli waigizaji wengi kwa sasa hujivalia tu mavazi hayo hata pasipostahili.


No comments:

Post a Comment