Pages

Friday, August 21, 2015

Umoja Wa Mashirikisho Ya Sanaa Tanzania Walaani Rais Kikwete Kuagwa Kisiasa Na Kinyume Cha Taratibu Milimani City.


Tamko la Marais wa Mashirikisho ya Sanaa nchini
kuhusu kuagwa kwa
Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tarehe 19/08/2015 Ukumbi wa Habari Maelezo, Dar es Salaam.

Ndugu wanahabari,


Umoja wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania unaunganisha Mashirikisho yote ya sanaa nchini kama ifuatavyo:
  • Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA)
  • Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF)
  • Shirikisho la Sanaa za Maonesho Tanzania (TAPAF)
  • Shirikisho la Muziki Tanzania (TMF)

Mashirikisho hayo yanaundwa na vyama vya wasanii wa fani husika katika ngazi ya kitaifa, yamesajiliwa kwa mujibu wa sheria na chombo cha serikali chenye mamlaka ya kusimamia shughuli zote za sanaa nchini BASATA, kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Na. 23 ya Mwaka 1984 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Umoja wa Mashirikisho ya Sanaa unachukua fursa hii kuipongeza kwa dhati kabisa serikali yetu ya awamu ya nne chini ya uongozi madhubuti na uliotukuka wa Mhe. Rais Dtk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuonyesha nia njema na ya dhati kwa jitihada zake katika kuinyanyua tasnia ya Sanaa nchini na kwamba katika kipindi cha uongozi wake tasnia hii imefanikiwa kukua na kutambulika ndani na nje ya nchi kwa kiasi kikubwa sana.

Pia tunawapongeza watu binafsi, Makampuni, Taasisi na Mashirika mbalimbali ya ndani na nje ambayo kwa namna moja ama nyingine yameonesha nia ya dhati katika kuchangia kwa hali na mali maendeleo ya tasnia ya sanaa nchini.

Hata hivyo tunasikitika kuona kwamba kuna baadhi ya watu au makundi mbalimbali kwa makusudi kabisa wanaitumia vibaya nia njema ya Mhe. Rais kwa kutumia mwamvuli wa tasnia ya sanaa ambapo huwalaghai wasanii wachache kwa maslahi yao binafsi.

Ikumbukwe kwamba Tarehe 6/8/2015 kundi la watu waliyojiita Muungano wa Wasanii nchini, waliandaa tukio la kumuaga Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika ukumbi wa Mlimani City huku wakijua kwamba muungano au umoja huo hauko kisheria na hauna hadhi ya uwakirishi wa wasanii wote nchini.

Umoja wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania, unatambua haki ya watu au makundi tofauti katika kuandaa shughuli na matukio mbalimbali likiwemo tukio la kumuaga Rais wetu mpendwa, kama watanzania walikuwa na haki hiyo.  Tunachopinga hapa ni namna ambavyo watu hao wasiyo na nia njema na tasnia ya sanaa, kutumia mwamvuli wa wasanii wote kinyume cha utaratibu.

Ikumbukwe kwamba sanaa nchini ni pana kuliko uwakilishi wa kibaguzi ulifanywa katika tukio tajwa, kwa mujibu wa tafsiri ya Baraza la Sanaa la Taifa; sanaa imegawanyika katika maeneo makuu manne kama ifuatavyo:
  • Sanaa za Ufundi
  • Sanaa za Filamu
  • Sanaa za Maonesho na
  • Sanaa za Muziki
Tukio lile siyo tu limekiuka matakwa ya kisheria kwa kutumia jina ambalo halijasajiliwa, wandaaji kumdanganya Mhe. Rais kwa kujifanya wao ndiyo wawakilishi halali wa wasanii nchini, lakini pia limeleta sintofahamu na mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wasanii wote wa sanaa zote nchi nzima.

Umoja wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania, tumesikitishwa sana na tunalaani vikali kitendo kile na tukiwa ni viongozi halali wa Mashirikisho ya Sanaa nchini na wasemaji wa wasanii wa sanaa zote tunatamka wazi na tunaomba jumii ya wasanii wa sanaa zote, wapenda sanaa na maendeleo ya sanaa na watanzania wote kwa ujumla kwamba; hatulitambui tukio lile na kwamba Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amedanganywa na kwamba bado hajaagwa rasmi na wasanii wote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tunachukuwa fursa hii kuishauri serikali ya awamu ya nne na awamu zijazo kuwa makini na wajanja wachache wanotumia majina ya makundi mbalimbali katika jamii kwa maslahi yao binafsi, ni vyema Rais wa nchi kama taasisi ikatumia mfumo wa kiitifaki ambao imejiwekea ili kuwafikia walengwa na kuziba mianya ya wajanja wachache wanaotumia, ukarimu, ukaribu na nia njema ya viongozi wetu kwa manufaa yao binafsi.

Umoja wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania, tunatambua kampeni za uchanguzi zinaanza na kwa mbinu mbalimbali wasanii watatumika katika kufanikisha kampeni za wanasiasa, tuna wakumbusha wasanii wasitumike vibaya bali wafanye kazi yao kwa kufuata maadili ya nchi yetu, weledi mkubwa na kwa makubaliano maalum (Mikataba) walipwe vizuri bila kudhulumiwa. Tuwaombe watanzania wasiwe na nongwa wanapomuona msanii amepanda kwenye jukwaa la wanasiasa kwa kumnyooshea kidole, tutambue ya kwamba sanaa ni kazi kama kazi nyingine na kwamba msanii analipwa kama wanavyolipa mafundi mitambo na watu wengine katika matukio hayo.

Mwisho tunawasihi wasanii wote nchini wawe watulivu na wasiyumbishwe na watu wachache wenye nia ya kutugawa, tudumishe ushirikiano wetu katika kuendeleza harakati za kupambana na mifumo dharimu iliyokithiri dhidi ya tasnia yetu.

Mungu ibariki tasnia ya sanaa, Mungu ibariki Tanzania, Ahsanteni kwa kutusikiliza.

Imetolewa na

………………………………………………………………
Kimella Billa
Mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Mashirikiso ya Sanaa
kwa niaba ya

Marais wote wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania

No comments:

Post a Comment