Pages

Tuesday, December 9, 2014

Serikali Inashirikiana Na Maharamia Kuendelea Kuwafanya Wasanii Wawe Maskini Nchini !: Ignas Mkindi

Rais wa TAFF Simon Mwakifwamba na wasanii wa filamu Tanznaia
Makala hii fupi imeandikwa na Ignas Mkindi ambaye ni mwandishi wa miswada ya filamu na mmoja wa wapiganaji wakubwa katika tasnia ya filamu nchini.


SERIKALI INATUTIA UMASIKINI

"Mara nyingi tumekuwa tukiwasikia viongozi wa serikali wakihamasisha wasanii kujiunga katika vikundi hasa kuanzisha SACCOSS ili kuweza kupata fursa ya mikopo kwa ajili ya kuongeza uwezo katika kufanya kazi zao na kujiinua kiuchumi.
Ni wazo zuri sana na naliunga mkono. 


Kuna kauli pia ya kutaka wasanii kujiendeleza kielimu ili kuweza kufanya kazi bora zitakazoweza kuvuka mipaka ya nchi yetu. Pia ni wazo kubwa la kimaendeleo na naliunga mkono. 
Miaka michache iliyopita serikali hii yetu kwa nia njema kabisa iliamua kurasimisha filamu na muziki ili viweze kuendeshwa kibiashara zaidi na kuweza kuwafanya wadau wa tasnia hizo wakopesheke. Ila kubwa zaidi lililokuwa linanadiwa ni kuwa urasimishaji utazifanya kazi hizo zilindwe.
Suala hilo liliamsha matarajio makubwa kwetu tuliojiajiri katika tasnia hizi hasa ujio wa TRA ambayo iko katika kila kona ya nchi na ina nguvu kubwa kifedha.
Tukajua kuwa umefika wakati wa kuneemeka kutokana na kazi zetu. Tukajua hata wale waliokata tamaa wangerudi ili tule matunda ya kazi zetu. Sasa ni takribani miaka miwili, hali imezidi kuwa mbaya.


TRA tuliyemtegemea kawekwa mfukoni na maharamia, hafurukuti wala hapigi yowe. Kariakoo imeshindikana, Ubungo, Manzese, Yombo, Buguruni, Tandika, Mbagala, Unguja n.k biashara ya kazi haramu inaendelea kama kawaida huku TRA ikiwatisha wasambazaji halali wa kazi zetu kuwa watakiona cha moto wasipobandika stempu kwenye kazi zao.
Kila msanii sasa analipa kodi na hakuna tunachokipata zaidi ya kupata hasara ya kulipia kodi.
Serikali inatuhamasisha tujikusanye ili tupate mikopo, ishafikiria tutailipaje wakati kazi zilizojaa sokoni ni haramu? Au inaataka mpate sababu kuwa wasanii wakikopeshwa hawalipi?
Viingozi wanaotuambia tujiendeleze kielimu, muda gani tutajifunza wakati mchana kutwa usiku kucha tunalinda kazi zetu zisiibiwe?


Siamini kama serikali ina nia thabiti ya kuwakomboa wasanii, ninachoona ni maneno matamu ili wawasaidie kujaza wananchi wakati wa kampeni zenu.
Sina shaka kabisa kuwa serikali ndiyo inafanya wasanii nchini kuwa masikini kwa kuwa imechukua jukumu la kulinda kazi za sanaa halafu inakula na wezi wakati wasanii wamewaamini.
Tunahubiri kila siku kuwa wasanii wasiuze hakimiliki, mmechukua hatua gani kuzilinda haki hizo?
Kama Wasambazaji wana mtaji mikubwa na mitandao mipana lakini wanaibiwa, leo msanii ataweza kulinda ili arudishe mtaji wake achilia mbali faida?


Tufanye vita ya ukombozi, tupigane kwa ajili yetu na vizazi vyetu, tuungane kwa pamoja kusema hapana. Imefikia wakati wadau wote wa filamu na muziki tuisusie serikali, tuwasusie shughuli zao zote, kampeni zao zote za kisiasa hadi itakapotendea haki kodi yetu, itakapotusafishia soko letu, itakapolinda kazi zetu au ITAKAPOKIRI IMESHINDWA ILI TUJUE TUCHUKUE HATUA GANI"


                                                                Ignas Mkindi

No comments:

Post a Comment