Wednesday, February 19, 2014

TUZO ZA WATU(TANZANIA PEOPLE'S CHOICE AWARDS) ZAANZISHWA.

Mwaka 2009, wazo jipya lilizaliwa. Wazo la kuwa na tuzo zitakazopatikana
kwa mchakato wa wazi utakaotokana na mapendekezo ya watu wenyewe ya
kuchagua mastaa wa michezo, muziki, filamu au vipindi na watangazaji
wanaopendwa zaidi. Wazo hilo liliendelea kuboreshwa na mwaka huu (2014),
limeiva na liko tayari kutoka kwenye hatua ya wazo la kichwani, na kuwa
tukio lenyewe.

“Nilizisajili na kuanzisha mwaka 2009 ila kutokana na mipango na malengo
ya kampuni niliamua kuziweka kwanza hadi sasa,” anasema Mwenyekiti wa
Bongo5 Media Group, Luca Neghesti. “Sasa hivi tumeshuhudia ukuaji katika
tasnia mbalimbali na tumeona ni wakati muafaka wa kuwatunuku wale
wanaopendwa na wananchi, kuwapatia tuzo pamoja na zawadi ya fedha taslimu
milioni 1″ ameongeza.

Tofauti na tuzo zingine, tuzo za watu hazitafuti ubora bali zinalenga
wanaopendwa zaidi na tuzo hizi hazitajikita katika tasnia moja peke yake.
Kwa kuanzia, tuzo hizi zitatolewa katika tasnia ya burudani inayojumuisha
filamu na muziki. Pia zitaiangazia sekta ya utangazaji kwa kuwatunuku
watangazaji na vipindi vinavyopendwa zaidi na watu nchini huku pia
mwanamichezo bora (soka, basketball, ndondi na michezo mingine) naye
akipewa nafasi.

Tuzo za watu si tuzo za vijana peke yake, zipo kuwakilisha watu wa rika zote.
Tofauti nyingine kubwa ni kuwa tuzo za watu zitalenga kuwatunuku watu
kutokana na umaarufu ama kupendwa kwao na si ubora. “Tuzo hizi hazileti
ushindani na tuzo zingine kwasababu hazilengi tasnia moja tu,” anafafanua
Neghesti.
“Tanzania imesifiwa kwa uhuru wa vyombo vya habari na tuzo hizi zinalenga
kujumuika na tuzo zingine kuhakikisha watanzania wanaopendwa na kufanya
vizuri wanatambuliwa.”

Upigaji kura unaanza wiki hii katika vipengele 11 ambapo wananchi wenyewe
watachagua majina ya washiriki watakaoshindana kwenye vipengele hivyo.
Awamu ya kwanza ya upigaji kura itafungwa baada ya wiki mbili kutoka siku
ya kwanza ya upigaji kura na majina ya watu watano waliotajwa zaidi kutoka
kwenye kila kipengele watachaguliwa kama watajwa wa mwisho.
Kuanzia hapo, upigaji kura wa wananchi utajikita tu katika orodha ya
majina hayo matano kwenye kila kipengele kinachoshindaniwa. Wiki moja
baada ya majina ya washiriki kutangazwa, mchujo wa kwanza utafanyika
katika kila kipengele na mtu mmoja ataondolewa.


Wiki moja baadaye, mchujo wa pili utafanyika na kuwabakiza washiriki
watatu kwenye ila kipengele.
Washiriki wote 33 (watatu katika kila kipengele) waliosalia baada ya
kufanyika mchujo wa mwisho, watakuwa wageni wa heshima kwenye utoaji wa
tuzo hizo, utakaofanyika wiki moja baada ya mchujo huo wa mwisho. Katika
hafla hiyo, washindi watatangazwa na kila mshindi atapokea zawadi ya fedha
taslimu, shilingi 1,000,000 za Kitanzania pamoja na tuzo ya thamani
iliyotengenezwa kwa mkono kutoka kwenye mali ghafi asili za Kitanzania.

Tuzo za watu mwaka 2014 zitajumuisha vipengele 11 ambavyo ni pamoja na:

1. MTANGAZAJI WA REDIO ANAYEPENDWA (tuma SMS yenye ‘TZW1 na jina’ kwenda
15678)

2. KIPINDI CHA REDIO KINACHOPENDWA (tuma SMS yenye ‘TZW2 na jina’ kwenda
15678)

3. MTANGAZAJI WA TV ANAYEPENDWA (tuma SMS yenye ‘TZW3 na jina’ kwenda 15678)

4. KIPINDI CHA TV KINACHOPENDWA (tuma SMS yenye ‘TZW4 na jina’ kwenda 15678)

5. MWANAMICHEZO ANAYEPENDWA (tuma SMS yenye ‘TZW5 na jina’ kwenda 15678)

6. MWANAMUZIKI WA KIUME ANAYEPENDWA (tuma SMS yenye ‘TZW6 na jina’ kwenda
15678)

7. MWANAMUZIKI WA KIKE ANAYEPENDWA (tuma SMS yenye ‘TZW7 na jina’ kwenda
15678)

8. WIMBO UNAOPENDWA (2013) (tuma SMS yenye ‘TZW8 na jina’ kwenda 15678)

9. MUIGIZAJI WA FILAMU WA KIUME ANAYEPENDWA (tuma SMS yenye ‘TZW9 na jina’
kwenda 15678)

10. MUIGIZAJI WA FILAMU WA KIKE ANAYEPENDWA (tuma SMS yenye ‘TZW10 na
jina’ kwenda 15678)

11. FILAMU INAYOPENDWA (2013) (tuma SMS yenye ‘TZW11 na jina’ kwenda 15678)
JINSI YA YA KUPIGA KURA

Mchakato wa kupendekeza majina ya washiriki katika tuzo hizi utafanyika
kwa njia kuu mbili. Ya kwanza ni kwa kutumia tovuti ya  tuzo hizi ambayo
ni www.tuzozetu.com ambapo utakutana na hatua rahisi ya kupendekeza na
kutaja majina katika vipengele vyote 11.  Jinsi ya kupiga kura, bofya
palipoandikwa  Piga Kura na ufuate hatua rahisi kabisa ambayo haikuhitaji
kujiandikisha jina wala email yako.

Njia ya pili ni kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu ambapo utaandika neno
‘Tuzo’ kwenda namba 15678. Ukishafanya hivyo utaletewa Menu yenye
vipengele vyote 11 vikiwa na code number zake. Kutaja ama kupendekeza
jina, tuma code husika na jina kwenye namba hiyo hiyo; kwa mfano  Justin
Bieber. Gharama ya sms ni ile ile inayotozwa sms ya kawaida.

No comments:

Post a Comment