MILLEN
MAGESE ACHANGIA UJENZI NA VIFAA VYA SHULE
MWANAMITINDO mahiri wa kimataifa ambae pia aliwahi kuwa
Miss Tanzania 2001, Millen Happiness Magese amewagusa wakazi wa Mtwara kufuatia
ziara yake ya kimafanikio aliyoifanya mkoani humo na kukabidhi misaada
mbalimbali.
Millen ambae kwa sasa anaishi nchini Marekani
akijishughulisha na fani ya mitindo akiwa Mtwara alipokelewa na viongozi
mbalimbali wakiwamo Mkuu wa Wilaya ya Mtwara; Mhe. Willman Ndile, Mkuu wa Mkoa
wa Mtwara; Mhe. Simbakali na Mbunge wa Mtwara mjini; Mhe. Hasnain Murji.
Millen alitoa fedha taslim kiasi cha shilingi milioni 15
ambapo milioni 10 ilikuwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi ya Mjimwema
baada ya kutembelea shule hiyo na kuguswa na hali ya mazingira magumu
aliyoyakuta katika shule hiyo iliyopo kata ya Magengeni.
Millen awali alikuwa ametaka kupeleka msaada wake huo
katika shule ya msingi ya LiLilungu iliyopo Mtwara mjini lakini alijikuta
akimwaga milioni kumi kwa shule ya Mjimwema na kuongeza milioni tano kwa ajili
ya madawati ya shule ya Lililungu kwani awali alikuwa ameahidi kutoa milioni
kumi.
Shule hiyo yenye madarasa mawili yaliyojengwa kwa udongo
ambapo wanafunzi wakiwa ni wengi huku wengi wao wakiwa hawana viatu na sare zao
za shule zikiwa zimechakaa.
Akizungumza shuleni hapo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya
Mtwara Ndile, Millen alisema kuwa akiwa kama mwanamitindo ameguswa na hali
mbaya ya mazingira ya shuleni hapo hasa ikizingatiwa kuwa wanafunzi wanasomea
katika shule ya udongo huku wakiwa na mazingira duni ya kufundishia.
Aliongeza na kusema, "Mwaka 2001/2002 nilitembelea
mkoa wa mtwara ambao ulinigusa sana kwenye swala zima la elimu haswa mazingira
ambayo yanamfanya mtoto akae chini. Na nikaahidi siku moja mungu akijalia nitarudi
Mtwara na nimesikitika ni miaka 12 sasa bado watoto wanakaa chini nikaone
nirudi kutimiza ahadi na kutoa hamasa kwenye swala hili la elimu Mkoani mtwara”;
mbali na milioni kumi na tano pia aliahidi kuwatafutia sare za shule wanafunzi
hao jozi mbili kila mmoja na pia alikubali kuwa mlezi wa shule hiyo.
Pia alipata fursa ya kukaa na wajasilimali
walioandaliwa semina na mkuu wa wilaya pamoja na mbunge wa Mtwara mjini kujadili
mbinu za kuwaongezea kipato na kwa kuanzania milioni sita iliyopatikana
iligawanywa kwa wajasiriamali kulingana na vikundi ili wao watengeneze madawati
kwa ajili ya watoto wao, ambapo milioni tano ilitolewa na Millen Foundation na
milioni moja ilitolewa na Mhe. Murji
Naye mkurugenzi wa manispaa alisema Millen ameweka
historia kwani kitu hiki hakijawahi kufanyika Mtwara na mtu binafsi wanaangalia
ni jinsi gani Millen Magese atakumbukwa kama muanzilishi wa ujenzi wa shule ya
mji mwema.
Baada ya kuzungumzia ahadi yake hiyo Millen aliwahamasisha
wadau wengine aliiongozana nao kuchangia mchango wa shule hiyo akiwamo Mbunge
wa Mtwara mjini Murji ambae aliahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya
kufanikisha ujenzi zaidi wa shule hiyo na shilingi milioni moja kwa ajili ya
madawati.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara; Mhe Ndile pamoja na Mhe. Murji
waliwataka wananchi kuhamasika zaidi kwa kuunga mkono harakati za Millen katika
kuimarisha elimu mkoani humo kwa kuwa ameonesha mfano mzuri akiwa kama
mwanamitindo.
"Shukrani za dhati kwa Lucy Tabasamu kwa kutupa habari kamili"
No comments:
Post a Comment