Tuesday, January 29, 2013

BASATA INAKWAMISHA MAENDELEO YA SANAA NCHINI !

MARA nyingi nimekuwa nikiona wadau wakijitokeza na kutaka kuandaa matamasha au tuzo na mwishowe vitu hivyo uishia hewani bila ya kuendelea, japo vitu hivyo huwa ni chachu na vichocheo vya wasanii na kuwatia moyo hamasa katika ufanisi wa kazi zao, hakuna anayejali hayo lakini nimegundua shida ni taasisi zinazoshikilia wasanii kama ilivyo BASATA. Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ukisikiliza kauli mbinu zao ni kukuza sanaa, kusaidia wasanii ikiwa na kulinda utamaduni wa Taifa hili jambo ambalo kwangu ni tofauti na hisia zangu kuhusu taasisi hiyo, kuna madudu mengi ambayo yanaonekana, lakini kwa leo sitaongelea hayo zaidi ya kuongelea tuzo kwa wasanii wa filamu ambazo kila muandaaji anapojitokeza ukwamishwa.
Mwaka jana alitokea mdau mmoja na kuamua kuandaa tuzo kwa wasanii wa filamu Swahiliwood, tuzo hizo ziliitwa Bantu film Awards na kuzinduliwa katika Hotel ya Serena kwa gharama kubwa, tuzo hizo zilihudhuriwa na wasanii nyota katika tasnia ya filamu Swahiliwood na kupokelewa kwa furaha kubwa huku wasanii wakiamini kuwa kazi zao zinaanza kutambuliwa na kupewa heshima. Lakini bila kutegemea tuzo hizo ziliyeyeuka kama Saruji na wasanii wakaendelea kubaki kama watoto yatima wasiojua hata thamani yao katika jamii kwa zaidi ya miaka 6 sasa hakuna tuzo zozote zilizofanyika kwa ajili ya kuwapongeza wasanii ukitoa tuzo zisizo rasmi ambazo utolewa katika tamasha la Ziff Zanzibar ambazo hazijawekewa mizengwe. .
Kwa mara ya mwisho tuzo zilikuwa ni tuzo za Vinara ambazo kwa sasa zimesimama na kushindwa kuendelea pengine kutokana na gharama kuwa kubwa katika maandalizi ambazo kama unakosa mdhamini mtayarishaji unaweza kujikuta ukiingia katika madeni makubwa bila sababu ya msingi huku taasisi kama BASATA wakishindwa kukusaidia kwa lolote zaidi ya kutaka kutengeneza fedha kwa kigezo cha sheria. . Tuzo ni sehemu ya kuwatangaza (Promotion) wasanii na kazi zao sasa unapomwambia mtayarishaji alipe gharama 1,705,000/ ili apate kibali cha kuandaa hizo tuzo kuna nia ya kweli kuwasaidia wasanii au hawa wasanii ndio vitega uchumi vyenyewe ambavyo vinakamliwa maziwa hata bila ya kulishwa majani bora? Baada ya kuona hayo mtandao wa mahiri wa filamu Swahiliwood www.filamucentral.co.tz ukamua kuwatumia wadau na wapenzi wa filamu Bongo kuwachangua wasanii wao kupitia mitandao kisha kuwapatia tuzo wasanii husika baada ya BASATA kuona matangazo tu wakatuita tulifika na kuwaeleza nia yetu lakini wao walibaki na misimamo yao ya ajabu ya kuzuia tusiendelee na mchakato huu. Ikumbukwe kuwa mwaka 2011 tulijipanga kutoa tuzo kubwa na za kihistoria BASATA wakatuzuia kwa madai kuwa kuna muandaaji waliyemsajili kwa hiyo hawezi kutupa sisi kibali lakini hayo yalifanyika hata bila kutupa fursa kuonyesha vigezo vitu kama vinashabiana na muandaaji wao bali mhusika alionyesha dharau na ukiritimba uliopo katika taasisi hiyo. .
Tunapenda kurudisha suala hili kwenu wasanii na wadau wa filamu katika hali kama hiyo tutaendelea, tasnia ya filamu kwa sasa ina zaidi ya miaka 14 hakuna tuzo zozote kwa wasanii wetu, jambo linanalonishangaza ni kuzuia wengine kutoa hizo tuzo wakati nchi nyingine kuna kuwa na tuzo zaidi ya 50 iweje Tanzania watu wazuiwe kwa sababu kuna mtu kasajili na kufungia makabarasha chumbani kwake? Tunachukua nafasi hii kuwataka radhi wapenzi wetu kushitisha BORA ZA 2012 kwa muda hadi muafaka utakapopatikana kwa sababu iliyo nje ya uwezo wetu hizo ndio taasisi zinazokuza sanaa na kuwatangaza wasanii Tanzania.(source:filamucentral.co.tz)

No comments:

Post a Comment